Kocha Mkuu wa Simba SC Franco Pablo Martin anaamini licha Kiungo Mshambuliaji kutoka nchini Ghana Bernard Morrison kupewa mapumziko hadi mwishoni mwa msimu huu, bado kikosi chake kitakua na nguvu ya kuendelea kupambana katika michezo iliyosalia.
Uongozi wa Simba SC ulithibitisha kumpa mapumziko Kiungo huyo Ijumaa (Mei 13), huku mkataba wake ukitarajia kufikia kikomo mwishoni mwa msimu huu.
Kocha Pablo amesema hana budi kuheshimu maamuzi yaliyochukuliwa na Uongozi wa Simba SC kuhusu Morrison, lakini anaamini kikosi chake kitaendelea kuwa imara na kupambana hadi mwisho wa msimu huu.
Amesema Simba SC ina wachezaji wengi waliosajiliwa kwa ajili ya kuipambana timu hiyo ya Msimbazi, na yeye kama Kocha Mkuu atashirikiana nao bila kujali maamuzi gani yamechukuliwa kwa mchezaji mmoja kuondoka.
“Nadhani ni wakati sahihi wa kuheshimu uamuzi wa uongozi kwani Simba imesajili wachezaji wengi wenye uwezo wa wapo tayari kushindana muda wote na wana uwezo wa kuhakikisha tunashinda,” amesema Pablo na kuongeza
“Jambo lingine zuri kwa timu kulikuwa na wachezaji wengi majeruhi ila wamerejea kama Sadio Kanoute na Taddeo Lwanga wataongeza nguvu katika kikosi.”
Simba SC inajiandaa na mchezo wa Mzunguuko wa 24 wa Ligi Kuu dhidi ya Azam FC utakaorindima keshokutwa Jumatano (Mei 18), Uwanja wa Azam Complex jijini Dar es salaam.
Simba SC inakwenda kwenye mchezo huo baada ya kujihakikishia kucheza Nusu Fainali Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’ kwa kuifunga Pamba FC mabao 4-0, Uwanja wa Benjamin Mkapa juzi Jumamosi (Mei 14).