Kocha Mkuu wa Simba SC Franco Pablo Martin amesema wachezaji wake hawakucheza vizuri katika Kipindi cha kwanza dhidi ya ASEC Mimosas, hatua ambayo iliwapa nafasi wapinzani wao kupata mabao mawili ya kuongoza.
Simba SC ilikua mgeni wa ASEC Mimosas katika mchezo wa ‘Kundi D’, Kombe la Shirikisho Barani Afrika uliopigwa jana Jumapili (Machi 20), mjini Cotonou-Benin
Kocha Pablo amesema baada ya kuonyesha kiwango cha chini katika kipindi cha kwanza, kikosi chake kilibadilika wakati wa kipindi cha pili lakini kilishindwa kutumia nafasi za kufunga.
“Hatukucheza vizuri, ni tofauti na matarajio yetu, kipindi cha kwanza ASEC walitawala mchezo na kupata mabao mawili cha pili tulirudi na tulipiteza nafasi za kufunga,” anasema Pablo huku akisisitiza vijana wake wanatakiwa kupambana zaidi ya jana Jumapili (Machi 20) katika mchezo wa mwisho dhidi ya USGN.
Amesema kipindi cha kwanza kilikuwa kigumu kwao kwa kuwa wenyeji wao walitawala huku akikiri makosa ya mchezaji mmoja mmoja na timu nzima kwa ujumla ndiyo yamepelekea matokeo hayo.
“Hatukucheza vizuri na kusababisha kupoteza mechi, kulikuwa na makosa na lazima yatugharimu hasa tukiwa ugenini,” amesisitiza Pablo.
Katika Msimamo wa ‘Kundi D’ Simba SC imeporomoka kutoka nafasi ya kwanza hadi ya tatu ikiwa na alama 07 sawa na RS Berkane ya Morocco inayoshika nafasi ya pili, huku ASEC Mimosas ikiongoza kwa kufikisha alama 09.
USGN inaendelea kuburuza mkia wa kundi hilo kwa kufikisha alama 05, baada ya kulazimishwa sare ya 2-2 dhidi ya RS Berkane jana Jumapili (Machi 20), ikiwa nyumbani Niger.
Michezo ya mwisho ya ‘Kundi D’ itachezwa April 03, ambapo Simba SC itakua nyumbani Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam kucheza dhidi ya USGN, huku ASEC Mimosas ikisafiri kulekea mjini Berkane-Morocco kupambana na wenyeji RS Berkane.
Mshindi wa kwanza na wapili katika kundi hilo watatinga hatua ya Robo Fainali ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika msimu huu 2021/22.