Kocha Mkuu wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC Franco Pablo Martin amesema ametumia muda mwingi kuwaandaa wachezaji wake pamoja na kutoa maelekezo ya matumizi ya VAR ambayo itatumika kwa mara ya kwanza Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Simba SC itaikabili Orlando Pirates kesho Jumapili (April 17), katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, huku Mashabiki na Wanachama wake wakiwa na matuimaini makubwa na timu yao kuibuka na ushindi.

Kocha huyo kutoka nchini Hispania amesema: “Itakuwa ni mechi ya kimbinu, nimewafundisha wachezaji wangu jinsi ya kuitumia VAR, wanatakiwa kuwa makini kutofanya makosa, lakini wanatakiwa kucheza mpaka mwisho wa tukio, bila kuhofu kuwa filimbi itapigwa au la.”

“Nimewaambia wacheze mpaka wasikie filimbi, kwa sababu unaweza ukauacha mpira kumbe wala hujaotea. Ni kwamba VAR ndiyo itaamua, kwani unaweza kujiona labda umeotea, ukafunga bao, kumbe VAR itaonyesha hukuwa umeotea, au ukaacha, kumbe hukuwa umeotea, nimezungumza nao kuhusu hilo,” amesema kocha Pablo na kuongeza.

“Nina kocha hapa wa makipa ameshawahi kuzifundisha timu za huko, kwa hiyo anaijua Orlando Pirates na ligi ya huko, nina mchezaji ambaye ameshacheza huko (Bernard Morrison), pia nina watu wanaokusanya taarifa, lakini ile ni timu kubwa ambayo wala hupati tabu sana kuifuatilia, kujua inatumia mfumo gani, wachezaji gani wa kuchungwa, kwa sababu inaweka sana taarifa zake kwenye mitandao ya kijamii, kwa hiyo ni rahisi kujua mbinu zake na nini tunatakiwa tufanye,” amesema Pablo.

Taarifa za ndani za klabu hiyo zinasema kuwa kocha huyo alikabidhiwa na viongozi wa Simba video tatu za Orlando Pirates ambazo imecheza hivi karibuni kwa ajili ya kuzifanyia kazi, ambazo ni dhidi ya JS Saoura ya Algeria, Al Hittihad ya Libya ambazo ni za Kombe la Shirikisho na moja ya mechi ya Ligi Kuu Afrika Kusini ya hivi karibuni.

Fadlu Davis: Ninajua ubora, udhaifu wa Simba SC
Namungo FC yamshughulisha Nesreddine Nabi