Kikosi cha Mabingwa wa Soka nchini Zambia Power Dynamos kipo jijini Dar es salaam kwa ajili ya mpambano wa Mkondo wa Pili wa wa Kuwania kufuzu Hatua ya Makundi Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Simba SC, huku kocha mkuu wa timu hiyo, Mwenya Chipepo akingiwa na hofu juu ya wapinzani wao.

Mchezo huo wa Mkondo wa Pili utakaopigwa keshokutwa Jumapili (Oktoba Mosi), kwenye Uwanja wa Azam Complex utatoa taswira nzima ya timu itakayosonga mbele katika hatua ya makundi ya michuano hiyo itakayoanza kutimua vumbi kuanzia Novemba.

Akizungumza jijini Dar es salaam, Chipepo amesema haitakuwa mchezo mwepesi kutokana na rekodi ya Simba, ingawa hawataingia kinyonge kwani kila mmoja wao anatambua umuhimu wa michuano hiyo mikubwa Afrika.

“Baada ya kumaliza mchezo wa mwisho sisi kama benchi la ufundi tulikaa na wachezaji na kuwajenga kimwili na kiakili kwa sababu wapo baadhi yao walishaanza kushawishika jambo ambalo kwetu halikuwa nzuri.” amesema.

Chipepo ameongeza changamoto katika mchezo huo ni nguvu kubwa ambayo mashabiki wa Simba SC wanayo kwani hata mechi ya kwanza Zambia waliliona hilo, hivyo wanatarajia ugumu kwenye mchezo marudiano.

“Ukizungumzia Afrika Mashariki nadhani Tanzania ina mashabiki ambao wako karibu zaidi na timu zao na hilo wamelionyesha kwa vitendo kwa sababu wamekuwa nazo bega kwa bega japo tuko tayari kukabiliana na kila hali.”

Mabingwa hao wa Zambia walifuzu hatua hiyo kwa bao la ugenini baada ya mchezo wa kwanza kupoteza mabao 2-1 dhidi ya African Stars ya Namibia kisha marudiao kwenye Uwaja wa Levy Mwanawasa ikashinda 1-0.

Mchezo wa Mkondo wa Kwanza dhidi ya Simba SC uliopigwa, Ndola Zambia na timu hizo zilifungana mabao 2-2 huku shujaa wa Mnyama akiwa ni Clatous Chama aliyefunga yote mawili, hivyo kuiweka timu yake kwenye mazingira nmazuri ya kutinga hatua ya makundi.

BMH kuimarisha upasuaji Mishipa ya Damu ya Ubongo bila kufungua Fuvu
Samuel Eto'o akalia kuti kavu Cameroon