Kocha Mkuu wa Simba SC, Roberto Oliveira ‘Robertho’ amesema anajivunia ushindi dhidi ya Tanzania Prisons kwa vile wachezaji wake walitumia mbinu alizowafundisha.
‘Robertho’ amesema hayo baada ya kutia kibindoni Point tatu za mpambano huo ambao uliunguruma katika Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya, huku akitamba kwa hivi sasa lengo lao ni kuchukua Pointi tatu katika kila michezo ya Ligi Kuu msimu huu.
“Ninawapongeza wachezaji wangu wamejituma na jambo la msingi kwetu ni kupata Pointi tatu,”‘alisema.
Katika mchezo huo, Simba SC iliendeleza ubabe mbele ya maafande wa Tanzania Prisons, baada ya jana Alhamis (Oktoba 05) kuibuka na ushindi wa mabao 3-1.
Kufuatia ushindi huo, Simba SC imefikisha Pointi 12 baada ya kucheza mechi nne za ligi hiyo na hivi sasa inaongoza msimamo wa Ligi Kuu.
Mabao ya Simba SC katika mchezo huo, yalipachikwa wavuni na John Bocco, Clatous Chama na Saido Ntibazonkiza, yalitosha kuwapa wekundu hao Pointi tatu za ugenini jijini Mbeya.
Msimu uliopita Simba SC walianza kushinda bao 1-0 katika mchezo wa kwanza kabla ya kuitandika Tanzania Prisons mabao 7-1 katika mchezo wa mzunguko wa pili.
Katika mchezo wa jana, mpira ulianza kwa kila timu kushambulia lango la mwenzake, dakika ya 14 ya mchezo, Edwin Barua, aliifungia Prisons bao la kuongoza baada ya kuzamisha wavuni moja kwa moja mpira wa adhabu aliopiga nje ya eneo la hatari.