Kocha Mkuu wa RS Berkane ya Morocco Florent Ibenge amesema hatashangaa kuiona Simba SC ikicheza Fainali ya Kombe la Shirikisho msimu huu, kufutia kiwango chao kuikarika madhubuti.
Simba SC jana Jumapili iliicharaza RS Berkane bao 1-0, katika mchezo wa ‘Kundi D’ Kombe la Shirikisho Barani Afrika, uliounguruma Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.
Ibenge ambaye aliwahi kuinoa timu ya taifa ya DR Congo ametoa kauli hiyto alipohojiwa na tovuti ya Goal.Com, ambapo amesema Simba SC imekua na kiwango bora katika misimu minne mfululizo waliyocheza Ligi ya Mabingwa Barani Afrika na sasa Kombe la Shirikisho.
Amesema hatua hiyo imeifanya klabu hiyo kuwa na kikosi imara ambacho kinaweza kupambana popote pale barani Afrika na kupata matokeo mazuri, hivyo hatashangaa kuona wakifika hatua ya Fainali ya Kombe la Shirikisho msimu huu.
“Simba SC kwa misimu minne sasa wamepata wasaa wa kucheza michezo migumu katika Ligi ya Mabingwa Afrika, imewajenga vyema hivyo kwa msimu huu kucheza katika kombe la Shirikisho naamini wanaweza kufika fainali na hata kuchukua ubingwa.”
“Simba SC wamejiandaa vizuri, ni wazi inaonesha wana kikosi imara na chenye malengo makubwa, hivyo nilitarajia upinzani tofauti.” amesema Ibenge ambaye hadi sasa hajui hatma ya kibarua chake huko RS Berkane.
Bao pekee na la ushindi katika mchezo huo ulioshuhudiwa na Mashabiki 35,0000 lilipachikwa wavuni na Kiungo Mshambuliaji kutoka nchini Senegal Pappe Ousman Sakho na kuifanya Simba SC kufikisha alama 07 kwenye msimamo wa kundi D.
Nafasi ya Pili kwenye msimamo wa kundi hilo inashikwa na ASEC Mimosas ya Ivory Coast yenye alama 06 baada ya kuifumua USGN mabao 2-1, sawa na RS Berkane inayoshika nafasi ya tatu, huku USGN ikishika nafasi ya 04 kwa kumiliki alama 04.
Michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika kwa kundi D itaendelea tena mwishoni mwa juma hili (Machi 20), ambapo Simba SC itakua ugenini ikicheza dhidi ya ASEC Mimosas nchini benin, huku USGN ikiikaribisha RS Berkane mjini Niamey-Niger.