Kocha wa Timu ya Taifa ya Wanawake Tanzania ‘Twiga Stars’, Bakari Shime, amesema sasa anaugeukia katika mchezo wa kuwania kufuzu Fainali za Afrika za Wanawake (WAFCON) dhidi ya Togo.
Kauli ya Kocha huyo imekuja baada ya kukiongoza kikosi chake kushinda ugenini dhidi ya Botswana juzi Jumanne (Oktoba 31) katika mchezo wa kuwania kufuzu Michuano ya Olimpiki 2024, itakayofanyika nchini Ufaransa.
Shime amesema anashukuru kuona amepata matokeo hayo na kusonga mbele kwa jumla ya ushindi wa mabao 3-0 baada ya ushindi wa mabao 2-0 walioupata nyumbani kisha wakashinda ugenini 0-1.
“Niwapongeze wachezaji wangu walipambana na kupata ushindi ugenini, walifuata maelekezo vizuri, wapinzani wetu walitumia nguvu na kasi kupiga mipira mirefu lakini tulicheza kwa mipango tuliyojiwekea na kuibua na ushindi huo,” amesema Shime
“Tumefanikiwa kuingia hatua ya tatu na sasa tutakutana na Afrika Kusini, lakini kabla ya kucheza nao tutakuwa na mapumziko mafupi na wachezaji wataenda kwenye majukumu ya klabu zao na mapema mwezi ujao tutajiandaa na mechi ya WAFCON dhidi ya Togo,”
Ameongeza wamepanga kuingia kambini mapema kujiandaa na mchezo dhidi ya Togo na watatumia kambi hiyo kurekebisha mapungufu aliyoyaona kwenye michezo iliyopita.
“Mchezo wa kufuzu Olimpiki umepita, sasa akili zetu tunaelekeza kwenye mchezo wa kufuzu fainali za Afrika, tunataka kupata ushindi ili kusonga mbele,” amesema Shime.