Kocha Mkuu wa Timu ya Soka ya Taifa ya Wasichana wa umri chini ya miaka 17 (Serengeti Girls), Bakari Shime, amesema kikosi chake kimedhamiria kuendelea kuipeperusha vyema bendera ya Tanzania katika fainali za Kombe la Dunia (U-17) zinazofanyika nchini India.
Serengeti Girls inatarajia kuivaa Colombia katika mchezo wa hatua ya Robo Fainali ya Kombe la Dunia utakayochezwa kesho Jumamosi (Oktoba 22) kwenye Uwanja wa Pandit Jawaharial Nehru, Goa.
Shime amesema wachezaji wake wanaendelea vizuri na mazoezi na tayari ameyafanyia kazi madhaifu aliyoyabaini katika mechi zilizopita ili wafanye vyema kwenye mchezo wa kesho.
Kocha huyo amesema ameiangalia michezo yote ambayo Colombia wamecheza, hivyo amejiandaa kuingia tofauti kwa lengo la kuwashangaza wapinzani hao.
Amesema mchezo huo utakuwa na ushindani mkubwa kwa sababu timu zote mbili zinahitaji kusonga mbele katika michuano hiyo inayoandaliwa na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA).
Amesema wamejipanga kucheza kwa tahadhari na nidhamu ili kujiondoa katika presha ya kuruhusu mashambulizi ya mara kwa mara ambayo yanaweza kuwaondoa mchezoni.
“Tunaendelea na maandalizi kwa ajili ya mechi yetu ya Jumamosi, tumefanyia kazi mapungufu yetu yaliyojitokeza katika mchezo uliopita na kuingia kwa tahadhari kubwa ili kufanikiwa kusonga katika hatua inayofuata, bado tunaamini tunaweza kufanya vyema zaidi,” Shime ameongeza.
Kocha huyo wa zamani wa Serengeti Boys, JKT Mgambo ya Tanga amesema anaendelea kuwapongeza wachezaji wake kwa hatua waliyofikia wakiwa wanashiriki kwa mara ya kwanza michuano hiyo kama nchi.
“Ushindani ni mkubwa sana na tuko makini, ninaimani na vijana wangu watapambana na kufuata maelekezo yote niliyowapa mazoezini, watatakiwa kuyahamisha katika mechi, hii itatusaidia na kutuweka salama, katika soka hakuna timu ndogo, Colombia nao wataingia wakifahamu wanakutana na timu iliyowaondoa mataifa makubwa,” Shime amesisitiza.