Kocha Mkuu wa Simba SC Roberto Oliveira Gonçalves do Carmo ‘Robertinho’ amesema Kikosi chake kitakuwa na kazi kubwa mbele ya Azam FC katika mchezo wa Nusu Fainali Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’.

Miamba hiyo ya Dar es salaam itakutana keshokutwa Jumapili (Mei 07) katika Uwanja wa Nangwanda Sijaona mkoani Mtwara kuanzia mishale ya saa Tisa alasiri, huku kila upande ukihitaji kushinda na kutinga Fainali ya ASFC msimu huu 2022/23.

Kocha Robertinho amesema amekuwa na maandalizi mazuri ya kikosi chake kuelekea mchezo huo, ambao anaamini utakua na kila aina ya upinzani kutokana na mfumo wa Michuano hiyo.

Robertinho amesema tangu walipoanza michuano ya ASFC msimu huu wamekutana na timu zenye nia ya kufanya vizuri ili zisonge katika hatua inayofuata, lakini bahati nzuri ilikuwa kwao na walishinda hadi kufikia Nusu Fainali.

Amesema Azam FC ina malengo kama ya Simba SC ya kutwaa Ubingwa wa ASFC, hivyo keshokutwa Jumapili itaingia Uwanjani kwa kucheza soka la ushindani ambalo litatoa upinzani kwa wachezaji wake, ambao wanatarajiwa kuanza safari baadae leo Ijumaa kutoka Lindi kuelekea Mtwara.

“Tunakutana timu ambazo kila mmoja malengo yake ni kupata hili kombe sasa utaona ni kwa jinsi gani tunapaswa kucheza kwa tahadhari na umakini mkubwa tukihakikisha tunatumia nafasi vizuri tutakazozipata ili kufika fainali,” amesema Kocha huyo ambaye kwa sasa ametokea kuwa kipenzi cha mashabiki wa Simba SC

Timu hizo zinakutana huku Azam FC ikiwa na kumbukumbu ya kupoteza bao 1-0 katika hatua ya Nusu Fainali ya michuano hii msimu wa 2020/21, lililofungwa na mchezaji wake wa zamani, Luis Miquissone baada ya mabeki kuzembea.

Katika mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa CCM Majimaji mjini Songea Mkoani Ruvuma, Miquissone alifunga bao hilo dakika ya 89 baada ya mchezaji wa zamani wa timu hiyo, Bernard Morrison anayeicheza Young Africans kwa sasa kuanzisha kwa haraka mpira wa kutenga ‘Free-Kick’.

Majimaji FC yasubiri hukumu TPLB
Malipo fidia Bima ya amana wateja FBME ni zaidi ya Bilioni 2