Kocha Mkuu wa Simba SC, Roberto Oliviera ‘Robertinho’ amesema kuwa maandalizi ya michezo miwili ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Power Dynamos yanaendelea, huku akitumia muda huo kujipanga na mchezo wa ufunguzi wa Ligi ya Soka Afrika (AFL) dhidi ya ya Al Ahly ya Misri.
Simba SC ambao wanaanzia Raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika watatupa karata yao ya kwanza Septemba 16 kwenye Uwanja wa Levy Mwanawasa, nchini Zambia.
Kocha Robertinho amesema kuwa akili yao na nguvu wameweka kwa ajili ya michezo hiyo miwili mikubwa, ambayo inahitaji maandalizi makubwa na umakini wa hali ya juu.
“Maendeleo ya kikosi changu yananipa moyo tumebakiza majuma mawili kabla ya kwenda kucheza ugenini nchini Zambia licha ya kuwa tulishinda mchezo wa kirafiki naamini kwenye mchezo ujao watakuja kivingine ndio maana na sisi tunaangalia kuingia tofauti,” amesema Robertinho.
Amesema baada ya Droo kuchezeshwa na wao kupangwa na Al Ahly ni mchezo mwingine mgumu ambao pia maandalizi yake yanaanza sasa hawana muda wa kusubiri watautumia muda walio nao kujiimarisha zaidi.
Katika hatua nyingine kocha Robertinho ameridhika na kiwango kilichoonyeshwa na wachezaji wawili, Henock Inonga na Kramo Aubin ambao wametoka kwenye majeruhi na wameanza mazoezi.
Naye Meneja wa Habari na Mawasilino wa Simba SC, Ahmed Ally, amesema kuwa kutokana na ukubwa wa tukio hilo la Ligi ya Soka Afrika (AFL) wanatarajia kuanza kuuza tiketi mapema zaidi ili kuwapa nafasi wanasimba kushuhudia tukio hili la kihistoria.