Uongozi wa Klabu ya Simba SC umeripotiwa kuwa katika hatua za mwisho za kumpa mkataba Kiungo Mshambuliaji Hassan Dilunga ambaye alikuwa nje tangu kuanza kwa msimu huu.
Dilunga alikuwa nje kwa muda mrefu akiuguza majeraha ya goti aliyoyapata msimu uliopita kabla ya kupelekwa Afrika Kusini kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji.
Taarifa kutoka Simba SC zinaeleza kuwa kiungo alirejeshwa kikosini Simba kwa sharti kuangaliwa mazoezini na madaktari kabla ya Kocha Mkuu wa timu hiyo, Oliviera Roberto ‘Robertinho’ kuamua hatma yake.
Mtoa taarifa hizi amesema madaktari wamewathibitishia Bodi ya Wakurugenzi wa Simba, kiungo huyo amepona na yupo fiti kupewa mkataba mpya kwa ajili ya msimu ujao.
Ameongeza kuwa wakati madaktari wakithibitisha kupona kwa Dilunga, kocha Robertinho ameomba muda wa majuma mawili ya kumuangalia zaidi kiungo huyo, licha ya kuvutiwa na kiwango chake mazoezini.
“Uongozi ulionekana kumuhitaji Dilunga, ndio sababu ya kumpa nafasi ya kufanya mazoezi na timu katika msimu huu kambini licha ya mkataba wake kumalizika.
“Jopo la madaktari limethibitisha kupona kwa Dilunga ambaye tayari ripoti yake imekabidhiwa kwa uongozi. Hivi sasa suala lake lipo kwa kocha ambaye naye amevutiwa na kiwango chake, licha ya kumuongezea siku za kumuangalia zaidi,” amesema mtoa taarifa hizi
Akizungumzia hilo, Meneja wa Habari na Mawasilino wa Simba SC Ahmed Ally amesema: “Muda wa usajili bado, lakini fahamu Dilunga yupo nyumbani, suala lake lipo kwa uongozi.”