Kocha Mkuu wa Simba SC Roberto Oliveira ‘Robertinho’ amesema hana presha na timu ambayo anaweza kupangwa nayo kwenye hatua ya Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika na badala yake yupo bize juu ya namna ya kufanyia kazi makosa yaliyojitokeza katika michezo ya Hatua ya Makundi ili kuboresha kikosi chake.
Droo ya Robo Fainali ya Michaano ya Klabu inayoratibiwa na Shirikisho la Soka Barani Afrika (Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika) inafanyika kesho Jumatano (April 5, 2023) mjini Cairo, Misri kuanzia saa 02:30 usiku kwa saa za huko, sawa na 03:30 usiku kwa saa za Afrika Mashariki.
Robertinho amesema hawezi kuchaguzi mpinzani wa kukuna na kikosi chake katika Hatua inayofuata, na badala yake amejiandaa kumakbili yoyote atakayekutana naye.
“Hatuwezi kuchagua mpinzani wa kukutana naye, yeyote ambaye tutapangwa naye tutakabiliana naye, tunaweza kufanya maajabu na kushangaza Afrika, tutafanya maandalizi hatua kwa hatua, yapo ambayo tuliyaona kwenye makundi tutadili nayo ili kuweka sawa mambo kabla ya hatua ya Robo Fainali,”
“Siku zote nimekuwa na mtazamo chanya hivyo matarajio yangu ni makubwa, yaliyopita yamepita na kazi kubwa ni kuona vile ambavyo tunaweza kuwa bora maradufu hatua inayofuata, tupo pazuri nafikiri mashabiki wasubiri timu bora zaidi Robo Fainali.”
“Tumeshafanya kazi ya kurekebisha makosa na muda tulionao tutamalizia, naamini kwenye ubora wa timu na hilo litatimia,” alisema kocha huyo kutoka nchini Brazil
Robertinho amenukuliwa akisema; “Ni mpira wa miguu, ni wakati wa kuelewa kama hakukuwa na makosa leo labda mechi ingekuwa ya sare kwa sababu Raja alifunga kisha tukasawazisha na kisha kuna kitu kilifanyika ambacho sipendi kuzungumzia. Ni aibu, ni mpira wa miguu.”
Katika Droo ya Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, vinara wa makundi (4) ambao ni Wydad Casablanca, Raja Casablanca (Morocco), Mamelodi Sundowns (Afrika Kusini), Esperance de Tunis (Tunisia), watatenganishwa na wale ambao walimaliza nafasi za pili, Al Ahly (Misri), JS Kabylie, CR Belouizdad (Algeria) na Simba SC (Tanzania).
Kisha itachezeshwa Droo kati ya timu ambazo zipo chungu cha kwanza (vinara) na wale ambao walishika nafasi za pili, timu ambazo zilitoka kundi moja mfano Simba SC na Raja Casablanca hawatakutana hatua hiyo na hata zile ambazo zinatoka nchi moja.
Katika Droo ya nusu fainali, ambayo nayo itachezeshwa usiku huo, timu kutoka kundi moja au zile za taifa moja zinaweza kukutana dhidi ya nyingine.
Michezo ya kwanza itachezwa Aprili 15 na 16, na ile ya marudiano itachezwa Aprili 22 na 23, mwaka huu, Simba na timu nyingine ambazo zilishika nafasi ya pili kwenye makundi yao zitaanzia nyumbani na kumalizia ugenini ili kupata mshindi wa jumla.