Kocha Mkuu wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC Franco Pablo Martin anaamini Nahodha na Mshambuliaji wa kikosi chake John Raphael Bocco ataendelea kuwashangaza wadau wengi wa Soka la Bongo, baada ya kufanya hivyo wakati wa mchezo wa Kombe la Shirikisho Barani Afrika dhidi ya ASEC Mimosas ya Ivory Coast Jumapili (Februari 13).
Simba SC ilikua mwenyeji wa mchezo huo, Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, huku Mshambuliaji huyo akichangia ushindi wa bao la pili na la tatu kwa timu yake.
Kocha Pablo amesema anaamini Bocco ana uwezo mkubwa wa kupambana uwanjani, hivyo wadau wa Soka la Bongo wajipange kuona mambo mengi mazuri kutoka kwake kuanzia sasa.
Amesema anamuamini Mshambuliaji huyo licha ya kutompa nafasi ya kuanza kwenye kikosi cha kwanza mara kwa mara, lakini jambo hilo halimnyimi nafasi ya kuamini namna anavyoweza kuisaidia Simba SC katika harakati za kutetea Mataji ya Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho Tanzania Bara msimu huu 2021/22.
“Bocco alikua kwenye kipindi kigumu cha mpito cha kushindwa kutimiza majumu yake Uwanjani, lakini ninaamini bado ana uwezo mkubwa wa kucheza na kutupa matokeo kama ilivyokua dhidi ya ASEC Mimosas, ninajua kwamba anapenda kufunga na atafanya hivyo bila mashaka.”
“Ikiwa una mfungaji bora kama Bocco, hakuna haja ya kuwa na mashaka kwa kuwa muda upo na kuna masuala mengine ambayo yanatokea kama uchovu na ushindani kuwa mkubwa, hilo tumeliona na tumelifanyia kazi,” amesema Kocha huyo kutoka nchini Hispania.
Licha ya kuonesha uwezo mkubwa kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho Barani Afrika dhidi ya ASEC Mimosas, Bocco bado hajafunga kwenye michezo ya Ligi Kuu na Kombe la ShirikishoTanzania Bara msimu huu 2021/22.