Benchi la Ufundi la Singida Big Stars limeendelea na mkakati wa kuhakikisha kikosi cha klabu hiyo kinafanya vizuri katika mchezo wa Robo Fainali Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’ dhidi ya Mbeya City FC.
Timu hizo zitacheza mchezo huo kweshokutwa Jumapili (April 02) katika Uwanja wa Liti mjini Singida, huku Singida Big Stars ikiwa na hesabu kali za kuutumia vyema uwanja wake wa nyumbani.
Kocha Mkuu wa Singida Big Stars, Hans Pluijm amesema wamekuwa na maandalizi mazuri kuelekea mchezo huo ambao wameupa umuhimu mkubwa, hasa baada ya kupoteza muelekeo katika Mbio za ubingwa wa Tanzania Bara msimu huu.
“Haitojalisha tumecheza kwa staili gani lakini kwenye mchezo huu tunachohitaji ni matokeo kwenda katika hatua inayofuata.”
“Sisi tunahitaji ushindi na wenzetu tunajua watakuja kwa lengo la ushindi lakini tupo nyumbani na imani yetu ni kufanya vizuri,” amesema kocha huyo wa zamani wa Young Africans na Azam FC.
“Wachezaji wana kiu na lengo la ujumla la Singida ni kuvuka hatua hii na kwenda hadi fainali. Napenda sana timu za ushindani na presha kubwa na fainali nitazipata huko,” amesema Pluijm.
Mbali na mchezo huo wa Jumapili (April 02), pia ASFC itashuhudia mapambano mengine yatakayozikutanisha Simba SC na Ihefu, Young Africans na Geita Gold na Azam FC itamenyana na Mtibwa Sugar michezo yote ikipigwa jijini Dar es Salaam kati ya April 3, 7 na 8.
Michuano hiyo kwa sasa imekuwa na msisimko mkubwa huku Singida mastaa wake wakipania kwa udi na uvumba kupata nafasi yoyote ya kushiriki kimataifa mwakani, Iwe kwa Ligi au ASFC.