Kocha Mkuu wa Singida Big Stars Hans Van Der Pluijm amesema licha ya kubaki michezo minne ili msimu kuisha, lakini kwake binafsi hadi sasa mchezaji bora ni Mshambuliaji na Kinara wa ufungaji bora Ligi Kuu Bara Fiston Mayele.

Mayele alifunga bao moja juzi katika ushindi wa 5-0 dhidi ya Kagera Sugar na kumfanya kufikisha mabao 16 msimu huu akiifikia rekodi aliyoiweka msimu uliopita nyuma ya aliyekuwa mshambuliaji wa Geita Gold, George Mpole aliyefunga 17.

Kocha huyo kutoka nchini Uholanzi amesema kuna wachezaji wengi wamefanya vizuri, ila Mayele ameonyesha utofauti mkubwa.

“Kuona mchezaji anafunga mabao 15 na kuendelea kwa misimu miwili mfululizo sio jambo la kawaida na wengi wamekuwa hawana hicho kiwango. Ana spidi, anajua jinsi ya kujipanga, utulivu wake mbele ya lango la mpinzani na ni mmaliziaji mzuri,” amesema

Pluijm ameongeza kuwa kitu kingine kinachomtofautisha nyota huyo na wengine ni kutokuwa na majivuno kwani baadhi wakiona wamefanikiwa hujisahau, jambo linalowafanya kuzorotesha vipaji pindi tu wanapozoea mazingira ya sehemu husika.

Wakati Pluijm akisema hayo, Mayele ana kazi kubwa ya kufanya katika michezo mitano iliyobaki kwa Young Africans kwani kati ya hiyo ni timu mbili tu ambazo hajazifunga ikiwemo Simba anayokwenda kukutana nayo Jumapili (April 16) na mchezo wa mwisho dhidi ya Tanzania Prisons.

Katika michezo iliyobaki kwa Young Africans mbali na hiyo ni dhidi ya Singida Big Stars ambao tayari mchezo wa kwanza ameifunga mabao matatu (hat-trick) huku Dodoma Jiji na Mbeya City kila moja akiwa ameifunga mawili katika mzunguko wa kwanza.

Ben Chilwell achekelea mkataba mpya Chelsea
Ashikiliwa kwa kuchoma moto Maduka alipwe Bima