Kocha Mkuu wa Singida Big Stars, Hans Van der Pluijm, ameendelea kusisitiza mpango wa kuivurugia Young Africans, katika michezo miwili mfululizo itakayochezwa mjini Singida juma lijalo.
Singida itaanza kucheza na Young Africans Mei 4, katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kabla ya kucheza tena Mei 7, mwaka huu katika mchezo wa Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho Tanzania Bara, michezo yote itapigwa Uwanja wa CCM Liti, Mkoani Singida.
Kocha huyo kutoka nchini Uholanzi amesema atahakikisha kikosi chake hakifanyi makosa hata kidogo katika michezo miwili mfululizo itakayowakutanisha na mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu.
Amesema anafahamu Young Africans wana umahiri mkubwa katika kutumia nafasi wanazozitengeneza na anakiandaa kikosi chake kukabiliana na hali hiyo, ikiwezekana kuvuruga mipango yao ndani ya dakika 90.
“Nimekuwa nikiwafatilia Young Africans katika michezo ambayo imecheza ya ligi na michuano ya Kimataifa, nimewaona wapinzani wangu wazuri hasa kutumia makosa na kutafuta ushindi.”
“Hatuwezi kurudia makosa ya nyuma na tupo kwenye Nusu Fainali na tutacheza dhidi ya Young Africans, kila kitu kinawezekana na hakuna kinachoshindikana pale utakuwa unaamini kwamba unaweza kufanya kitu ndani ya timu yako,” amesema kocha huyo