Baada ya kukishuhudia kikosi chake kikichezea Bakora 2-0 mbele ya Mabingwa watetezi Tanzania Bara Young Africans, Kocha Mkuu wa Singida Big Stars Hans van der Pluijm, amesema hatakubali tena kufungwa na wababe hao wa Jangwani.
Singida Big Stars Jumatano (Mei 03) ilishindwa kufurukuta katika Uwanja wake wa Nyumbani CCM Liti kwa kukubali kupigwa kichapo hicho ndani ya dakika 20 za kipindi cha kwanza, na kupelekea kuzitema alama tatu muhimu.
Kocha Hans amesema kwenye mchezo ujao wa Kombe la Shirikisho la Tanzania Bara ‘ASFC’ hatakubali kikosi chake kupoteza tena mbele ya Young Africans, kwa sababu atahakikisha anajipanga vizuri ili kushinda mchezo huo na kutinga Fainali ya michuano hiyo.
Amesema hata ikitokea anatinga Fainali ya michuano hiyo, pia hatakuwa tayari kupoteza mbele ya Simba SC au Azam FC ambapo moja kati ya timu hizo itaingia Fainali baada ya mchezo wa Nusu Fainali ya ASFC utakaochezwa leo Jumapili (Mei 07) mjini Mtwara.
“Tulijipanga kushinda mechi zote mbili dhidi ya Young Africans, ila kwa kuwa tumefungwa huu hatutakubali kufungwa kwenye mchezo ujao tena, maana hamu yetu ni kuhakikisha tunacheza na fainali iwe na Simba au Azam atakae ingia,” amesema Plujm
Young Africans ilitarajiwa kucheza mchezo wa Nusu Fainali ya ASFC dhidi ya Singida Big Stars kesho Jumapili (Mei 07), lakini TFF imeusogeza mbele mchezo huo kwa kutoa nafasi kwa wawakilishi hao wa Tanzania kwenye Michuano ya Kimataifa kujiandaa vizuri kuikabili Marumo Gallants ya Afrika Kusini.
Taarifa zinaeleza kuwa mchezo huo umepangwa kuchezwa mwishoni mwa mwezi huu katika Uwanja wa CCM Liti mkoani Singida.