Kocha Mkuu wa SIngida Big Stars Hans Pluijm, amekataa kubebeshwa zigo la lawama baada ya kikosi chake kushindwa kufurukuta mbele ya KMC FC katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliopigwa Ijumaa (Mei 12).

Pluijm alishuhudia ubao wa Uwanja wa Uhuru ukisoma KMC 2-0 Singida Big Stars na kuwafanya wayeyushe pointi tatu mazima.

Kocha huyo kutoka nchini Uholanzi amesema wakati mwingine wachezaji wanakwama kutumia mbinu ambazo wanapewa kutokana na kushindwa kujitoa.

Pluijm ameweka wazi kwenye michezo ambayo imebaki watahakikisha wanapambana kupata matokeo chanya ili kufikia malengo waliyojiwekea.

Pluijm amesema: “Kuna wakati huwezi kusema matokeo yanapokosekana ni sababu ya benchi la ufundi, hapana, kuna muda unaota mbinu nzuri lakini wachezaji wanashindwa kutumia nafasi ambazo wanazitengeneza.

“Kwa yanayotokea ni kuangalia makosa na kufanyia kazi kwa ajili ya wakati ujao, bado tuna mechi mbili za kucheza, tutajitahidi kupata matokeo mazuri, ninaamini wachezaji watajitoa zaidi na kufanya vizuri.”

Palasa Chaurembo apeta TPBRC
Promota: Maandalizi yanakwenda vizuri sana