Vinara wa Msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara Simba SC, wanaendelea kujiweka sawa mjini Mbeya, tayari kwa mpambano wa mzunguuko wa 32 dhidi ya Tanzania Prisons. Mpambano huo umepangwa kuchezwa Juni 28, Uwanja wa CCM Sokoine jijini Mbeya.
Simba iliyo chini ya Kocha Mkuu, Sven Vandenbroeck itashuka uwanjani ikiwa na kumbukumbu ya kushinda mabao mawili kwa sifuri, yaliyojazwa kimiana na John Bocco kwenye mchezo wao dhidi ya Mbeya City.
Kocha Sven amesema mchezo dhidi ya Tanzania Prisons utakua mchezo mzuri na muhimu sana kwa kikosi chake, na anaendelea kufurahishwa na maandalizi ya kikosi, ambacho kimeweka kambi mjini Mbeya.
“Ni mchezo muhimu na mgumu kwetu hilo tunalitambua hivyo wachezaji wana kazi ya kusaka pointi tatu kutimiza malengo.” Amesema Sven
Wapinzani wao Tanzania Prisons wataingia uwanjani wakiwa na kumbukumbu ya kulazimisha sare ya kufungana mabao mawili kwa mawili dhidi ya JKT Tanzania, kwenye mchezo wao uliochezwa Uwanja wa Sokoine kati kati ya juma hili.
Mchezo wa duru la kwanza uliochezwa Uwanja wa Uhuru, Dar es salaam, Simba ilitoshana nguvu ya bila kufungana na Tanzania Prisons hivyo kazi itakuwa kubwa pale watakapokutana ndani ya uwanja CCM Sokoine.