Kocha Mkuu wa Mabingwa Tanzania Bara Simba SC Sven Vandenvroeck, amekamilisha maandalizi ya kikosi chake kuelekea mpambano wa Nusu Fainali Kombe La Shirikisho utakaowakutanisha dhidi ya Young Africans Uwanja wa Taifa, Dar es salaam Kesho Jumapili.
Simba SC waliwasili jijini humo juzi Alkhamis wakitokea Lindi kupitia Mtwara, na moja kwa moja walielekea kambini kuanza maandalizi ya mchezo huo ambao utaanza mishale ya saa kumi na moja jioni.
Kocha Sven amesema amekamilisha maandalizi ya kikosi chake na ana matarajio makubwa ya kuona matokeo chanya baada ya dakika 90 za mchezo huo, ambao utakua njia ya kuwafikisha Fainali Kombe la Shirikisho Tanzania Bara msimu wa 2019/20.
Kocha huyo kutoka Ubelgiji amesema anajua mchezo huo ni ngumu na ndio tegemeo pekee kwa wapinzani wao Young Africans kupata tiketi ya kushiriki michuano ya kimataifa msimu ujao, hivyo amewaandaa wachejai wake kupambana kufa na kupona ili kufanikisha azma ya ushindi.
Amesema wanahitaji kuongeza umakini na kucheza katika kiwango chao bora ili wapate matokeo chanya na hatimaye kuwaondolea machungu mashabiki wao wanaoumizwa na kipigo walichapata Machi 08, mwaka huu kutoka kwa watani zao.
“Tunahitaji kuwa makini na watulivu zaidi, mechi ya Jumapili ni mechi itakayokuwa na ushindani, changamoto mbalimbali pamoja na presha, tunatakiwa kutokuwa na papara, tunachotakiwa kufanya ni kutumia vema nafasi tutakazozitengeneza,” Sven alisema.
Naye Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Haji Manara, amesema wamejipanga kupata ushindi ili kuendelea na kampeni yao ya kuchukua vikombe msimu huu.
Manara amesema siri ya mafanikio ya timu yao msimu huu, imetokana na kuwa na kikosi imara ambacho kwa asilimia kubwa kitaendelea kuitumikia klabu hiyo tena katika msimu ujao.
“Tumejipanga, watatueleza walipataje ushindi Machi 8, au kama watabahatisha kwa mara nyingine, hawawezi,” Manara alitamba.
Mwamuzi wa kati wa mchezo huo atakuwa Aboubakari Mturo, ambaye atasaidiwa na Abdallah Mwinyimkuu, Nadeem Aloyce, Ramadhani Kayoko, Frank Komba na Kassim Mpanga huku Kamisaa akiwa ni Ally Katolila.
Simba ilifika hatua hiyo baada ya kuwaondoa waliokuwa mabingwa watetezi wa michuano hiyo Azam FC kwa kuwafunga mabao mawili kwa sifuri, wakati Young Africans ilisonga mbele kutokana na kuichapa Kagera Sugar magoli mabao mawili kwa moja, michezo yote ya hatua ya Robo Fainali ilichezwa jijini.