Kocha msaidizi wa timu timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ Hemed Morocco ameibuka na kutamka kuwa hawawaogopi wapinzani waliopangwa nao Kundi F, huku akitamba kuwa ndio wanaowataka.
Stars imepangwa na timu za Morocco, DR Congo na Zambia katika Fainali za Mataifa ya Afrika ‘AFCON 2023’ zitakazofanyika nchini lvory Coast mapema mwezi Januari 2024.
Kikosi hicho jana Ijumaa (Oktoba 13) Alfajili kilielekea Jeddah, Saudi Arabia ambacho kesho Jumapili kitacheza mchezo wa kirafiki dhidi ya Sudan.
Morocco amesema kuwa Kundi lao ni gumu walilopangiwa, na walitegemea hilo kutokana na timu zilizofuzu zote kuwepo katika viwango bora.
Kocha huyo ambaye pia ni Mkuu wa Benchi la Ufundi la Geita Gold FC amesema kuwa, licha ya ugumu wa Kundi hilo, lakini anaamini watafanya vizuri na kuandika rekodi ambayo haijawahi kuwekwa Tanzania katika michuano hii mikubwa Afrika.
Ameongeza kuwa kitu kikubwa kinachowapa faraja kupangwa na timu mbili za Zambia na DR Congo ambazo wamekutana nazo mara nyingi, kucheza michezo ya kirafiki na mashindano.
“Kitu ambacho kinachotupa matumaini ya kufanya vizuri katika Kundi F ni kupangwa na timu za Zambia na DR Congo ambazo mara nyingi tumekuwa tukicheza mechi za kirafiki na mashindano.
“Hivyo ninaamini kama tukijipanga vizuri, mwaka huu tutafanya vizuri na kufika katika hatua nzuri ya michuano hii.” amesema Morocco