Baada ya Tanzania Prisons kulazimishwa sare ya bila kufungana na Geita Gold FC, kocha mkuu wa timu hiyo, Fredy Minziro amesema ameridhishwa na kiwango kilichooneshwa na vijana wake.
Matokeo hayo yamewaweka maafande hao katika nafasi ya 12 kwenye msimamo na kufikisha alama saba katika michezo nane waliyocheza mpaka sasa kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara.
Akizungumza jijini Mbeya, Minziro amesema tofauti na mechi za awali ambazo walipoteza kwa sasa timu yake inacheza kwa uelewano mkubwa na kutengeneza nafasi za kutosha.
“Malengo yetu yalikuwa ni alama tatu lakini haikuwezekana, tunarudi kufanyia kazi mapungufu yetu ili tufanye vizuri kwenye mechi zijazo lakini nafurahishwa na mabadiliko ya kikosi changu kadri tunavyocheza mechi tunazidi kuimarika tofauti na ilivyokuwa mechi za mwanzo,” amesema Minziro.
Amesema ubutu wa safu ya ushambuliaji ambao umekuwa ukisababisha kupoteza nafasi nyingi ataendelea kulifanyia kazi.
Tanzania Prisons haijawa na mwendo mzuri katika misimu mitatu ya hivi karibuni na mara kadhaa imenusurika kushuka daraja na kuangukia kwenye mechi za mtoano.