Kocha Msaidizi wa timu ya taifa ya wanawake chini ya umri wa miaka 20, ‘Tanzanite Queens’, Esther Chabruma amekiri wana kazi ya kusuka kikosi cha timu hiyo kwa ajili ya mchezo wa kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya Nigeria.
Chabruma ametoa kauli hiyo baada ya Tanzanite Queens kufuzu kwa ushindi wa jumla wa mabao 12-0 dhidi ya Djibouti, huku akibainishwa kuwa kazi ya kujiandaa na mchezo dhidi ya Nigeria imeanza hivyo hawana muda wa kusherehekea.
“Hakuna mechi rahisi, Nigeria timu ngumu ukizingatia tuliwahi kukutana nao katika michuano ya Kombe la Dunia U-17, Tanzania tukaondolewa Robo Fainali na wao Nusu Fainali hivyo utaona ubora wao kazi yetu ni kuandaa kikosi kwenda kukabiliana nao,” amesema Chabruma.
Amesisitiza mwisho wa mchezo wa Djibouti ni mwanzo wa maandalizi ya mchezo ujao kuhakikisha wanafanikiwa kuipeleka Tanzania Kombe la Dunia inayotarajiwa kufanyika nchini Colombia, mwakani.
Katika mechi ya kwanza, Tanzanite ilishinda mabao 5-0 na mchezo wa pili ikashinda mabao 7-0, mechi zote zikipigwa Uwanja wa Azam Complex, Dar es salaam na hivyo Tanzanite kupenya hatua inayofuata kwa jumla ya mabao 12.