Baada ya Timu Taifa ya Soka ya Wanawake Tanzania, Twiga Stars kufanikiwa kutinga hatua ya pili ya kufuzu michuano ya Kombe la Mataifa Afrika Wanawake (WAFCON), Kocha Mkuu wa timu hiyo, Bakari Shime ameahidi kuendelea kufanya vizuri hadi wafuzu.
Twiga Stars juzi Jumanne (Septemba 26) ilifanikiwa kushinda kwa Penati 4-2 dhidi ya Ivory Coast katika mchezo wa marudiano wa kufuzu michuano hiyo baada ya matokeo ya jumla kuwa 2-2.
Mchezo wa kwanza ugenini, Twiga Stars ilipoteza kwa mabao 2-0, kisha juzi nyumbani ikashinda 2-0.
Shime amesema: “Kikubwa ni uvumilivu wa wachezaji wangu, tulikwenda mapumziko hatuna goli na tulikuwa nyuma kwa magoli mawili, lakini tulirudi kipindi cha pili na tumefunga magoli mawili, kisha tukashinda kwa Penati.
“Tunaenda raundi ya mwisho kucheza dhidi ya Togo, kila kitu kitakuwa vizuri, tutajitahidi kuhakikisha haturudii makosa kwenye raundi inayofuata.”
Twiga Stars sasa itacheza dhidi ya Togo katika raundi ya mwisho, ambapo mshindi wa jumla atafuzu kushiriki WAFCON, michuano itakayofanyika mwakani nchini Morocco.