Kocha Mkuu wa USGN Zakariou Ibrahim amesema ikitokea Simba SC imetuma ofa ya kutaka kumsajili Mshambuliaji wake kutoka nchini Niger, Victorien Adebayor hatakua na kinyongo chochote zaidi ya kumbariki Mshambuliaji huyo.
Simba SC inahusishwa na mpango wa kumsajili Adebayor, huku Uongozi wa Klabu hiyo uliwahi kusema upo tayari kumsajili mwishoni mwa msimu huu.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Salim Abdallh ‘Try Again’ alizungumza na Azam TV baada ya mchezo wa Mkondo wa kwanza dhidi ya USGN nchini Niger, ambapo alisema Adebayor ni mchezajio mzuri na wameanza mipango ya kuulizia kama anaweza kusajiliwa mwishoni mwa msimu huu.
Kocha Zakariou Ibrahim amezungumza na Dar24 Media kabla ya kuondoka jijini Dar es salaam leo Jumatatu (April 04) majira ya Alfajiri na kusema hana shaka na suala hilo, kwani Mshambuliaji wake ana uwezo mkubwa ambao unamuwezesha kucheza popote.
“Sina shaka na suala la kuondoka kwake, ikitokea Simba SC wapo tayari kumsajili waje kuzungumza na viongozi wetu na mambo yakishakuwa sawa nitampa baraka zote Adebayor ili aendelee kucheza soka lake kwa furaha.”
“Huyu mchezaji ana uwezo mkubwa sana kisoka, ana uwezo wa kucheza popote pale, suala la kuondoka ama kubaki kwa mchezaji ni kawaida kwa klabu yoyote duniani, mimi nipo radhi aondoke endapo Simba SC ama klabu nyingine inamuhitaji.”
“Naamini kama Simba SC wanahitaji huduma ya Adebayor, nina uhakika kikosi chao kitakua imara zaidi msimu ujao endapo atakua sehemu ya kikosi chao, kwa sababu ataongeza kitu katika safu yao ya Ushambuliaji.” amsema Zakariou Ibrahim
Zakariou Ibrahim amekua Kocha pekee katika Kundi D aliyeshindwa kuzifunga Simba SC na RS Berkane ya Morocco kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika, huku akiifunga ASEC Mimosas ya Ivory Coast pekee.
Simba SC ililazimisha sare ya 1-1 dhidi ya USGN nyumbani kwao Niger kabla ya kuichapa mabao 4-0 Dar es salaam, huku RS Bekakane ikipata sare ya 2-2 ugenini mjini Niamey na kushinda mjini Berkane mabao 5-3.