Kocha mkuu wa timu ya taifa ya England, Roy Hodgson amesema mshambuliaji Danny Welbeck atakuwa nje ya uwanja kwa miezi sita ijayo  baada ya kufanyiwa upasuaji wa goti.

Kauli hiyo ya Hodgson imewaumbua viongozi wa Arsenal ambao walishindwa kutaja muda sahihi ambao ulitarajiwa kwa mshambuliaji huyo kukaa nje ya uwanja baada ya kuthibitisha atafanyiwa upasuaji wa goti mwishoni mwa juma lililopita.

Kocha huyo wa England, amelazimika kuuweka wazi ukweli wa mambo alipokua kwenye mkutano na waandishi wa habari mapema hii leo, kwa lengo la kuuzungumzia mchezo wa kuwania kufuzu fainali za barani Ulaya za mwaka 2016 ambapo The Three Lion watapambana na Uswiz nyumbani.

Amesema ana wasi wasi mkubwa wa kumtumia mshambuliaji huyo kwenye fainali za Euro 2016, kutokana na muda anaotarajiwa kuwa nje ya uwanjani, hivyo hana uhakika kama atakua amesharejea katika kiwango chake cha kawaida.

Welbeck, mwenye umri wa miaka 24, amekua akijiuguza tangu April 26 mwaka huu na kwa mara ya mwisho alionekana uwanjani wakati wa mchezo wa ligi ya nchini England msimu wa 2014-15 ambapo Arsenal walikua akipambana dhidi ya Chelsea na kuambulia matokeo ya sare ya bila kufungana kwenye uwanja wa Emirates.

Unavyopaswa Kujibu Unapotakiwa Kuelezea Udhaifu Wako Kwenye Usaili Wa Kazi
Pogba: Nilikataa Kuihama Juventus