Kocha mkuu wa timu ya taifa ya Misri Shawky Gharib ameliweka njia panda suala la kumjumuisha mshambuliaji wa Liverpool Mohamed Salah, kwenye kikosi kitakachoshiriki michuano ya Olimpiki itakayounguruma mijini Tokyo, Japan baadae mwaka huu.
Gharib amesema suala la kumuita mshambuliaji huyo kwenye kikosi chake litategemea na maamuzi binafsi ya Salah, klabu ya Liverpool na meneja Jürgen Klopp, ambao anaamini wana mamlaka ya kusema neno la mwisho kabla ya benchi la ufundi kutangaza kikosi.
Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 27, ni sehemu ya wachezaji 50, ambao wapo kwenye kikosi cha Misri, kitakachofanyiwa mchujo hadi kufikia wachezaji 18 ambao watakwenda kushiriki michuano ya Olimpiki.
Wasi wasi wa kocha mkuu wa Misri, umekuja kufuatia tarehe za michuano ya Olimpiki kuingiliana na ratiba ya ligi kuu ya soka nchini England msimu wa 2020/21, ambayo imepangwa kuanza rasmi Agosti 08.
“Hatuwezi kulazimisha Salah awe sehemu ya kikosi, inatupasa kupata uhakika kutoka kwake, klabu yake na meneja wake, ambaye anapaswa kusema kama atamuhitaji katika maandalizi ya msimu mpya wa ligi,” alisema Gharib.
Gharib aliongeza kuwa: “Ushiriki wa Salah kwenye kikosi cha The Pharaohs bado unabaki katika maamuzi yake binafsi, naamini hata kama uongozi na meneja wa Liverpool watamkubalia, tunapaswa kusikilia nini atakachokiamua.”
“Tayari nimeshamteua kwenye kikosi changu cha wachezaji 50. Na kama mambo yatakwenda vizuri huenda akawa sehemu ya kikosi cha wachezaji 18 nitakacho kiwakilisha mwezi June.”
Michuano ya Olimpiki upande wa soka hushirikisha wachezaji wasiozidi umri wa miaka 23, lakini kanuni hutoa nafasi kwa kila timu shiriki kuwa na wachezaji watatu waliozidi umri huo.
Tayari FIFA imeshatoa nafasi kwa timu za taifa na klabu kukaa chini ili kufanya makubaliano ya kutumika kwa baadhi ya wachezaji kwenye michuano hiyo, huku klabu ikipewa kipaumbele cha kumruhusu ama kumkatalia mchezaji yoyote alieitwa kwa ajili ya kushiriki michuano ya Olimpiki.