Siku tano baada ya kampuni ya Promosheni ya Ngumi za Kulipwa nchini ‘PAFF’ kusema itafuata sheria kutokana na hasara walizopata katika pambano ambalo Bondia, Hassan Mwakinyo alisusa kucheza, Kocha wa bondia huyo, Amos Nkondo ‘Amoma’ amesema wako tayari kwa jambo hilo.
Kocha Amoma amesema itakuwa vema suala hilo litaenda ngazi ya sheria ili kufahamu nani alikuwa na makosa.
“Ujue katika mkataba kunakuwa na masharti ambayo mnakubalina baina ya pande mbili, hivyo kampuni ya PAFF ilingia makubaliano na Mwakinyo ila mwisho wa siku wakayavunja.
“Hivyo akienda katika sheria itakuwa vizuri kupata haki maana mahakama ndiyo sehemu ya kutafsiri sheria na kutoa haski,” amesema Amoma.
Oktoba 02 mwaka huu Mkurugenzi wa Kampuni hiyo, Godson Karigo ambaye ndiye Promota wa pambano hilo, alisema walipata hasara ya shilingi milioni 580 kutokana na Mwakinyo kushindwa kucheza.
Mwakinyo alitakiwa kucheza Septemba 29, mwaka huu kuwania Mkanda wa Ubingwa wa ‘IBA’ dhidi ya Julius Indongo kutoka Namibia. Pambano hilo, lilipangwa kuwa la raundi 12 la uzito wa kati.
“Hatukupata barua kutoka kwa Mwakinyo kama hatocheza ila zaidi ya kuona katika mitandao ya kijamii kupitia kurasa zake kuwa hawezi kupanda ulingoni, kutokana na hasara hizi tunafuata sheria zaidi,” alisema.
Karigo aliongeza kuwa Mwakinyo hadaiwi chochote kwani walishamaliza kila kitu kwa mujibu wa mkataba.
“Kuna watu wengi walikatisha safari kutokana na taarifa za Mwakinyo alizoweka katika kurasa zake za mitandao ya kijamii, kutokana tukio hilo tutafuata sharia inasemaje,” alisema Karigo.