Saa 24 baada ya kupangwa kucheza dhidi ya mabingwa wa soka Tanzania Bara Simba SC, kwenye mchezo wa hatua ya awali Ligi ya Mabingwa Afrika Kocha wa Plateau United, Abdul Maikaba ameelezea hofu yake.
Kocha Maikaba ambaye aliekiongoza kikosi chake hadi kufikisha alama 49 baada ya kucheza michezo 25 msimu wa 2019/20, kabla ya ligi hiyo kuvunjwa kufuatia janga la virusi vya Corona, ameelezea hofu yake kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter.
Maikaba ameandika: “Simba wana kocha mzuri, wanacheza soka la kushambulia kwa nguvu, wanapenda kumiliki mpira na hupenda kuwanyima nafasi ya kucheza wapinzani wao. Hivyo kwa kuwa tunaujua udhaifu wetu tutahakikisha tunajiandaa na kuwa tayari kuwakabili.”
Simba SC wataanzia ugenini katika harakati za kusaka ubingwa wa Afrika, dhidi ya Plateau United ya nchini Nigeria kati ya Novemba 27-29 na watarudiana jijini Dar kati ya Desemba kati ya 4-6.
Endapo Simba SC itafaulu mtihani wa kushinda michezo yake dhidi ya Plateau United iliyopewa namba 39, 40, itavaana na mshindi wa mchezo namba 37, 38 itakazokutanisha timu za CD do Sol ya Msumbiji dhidi ya FC Platinum ya Zimbabwe.