Kocha Mkuu wa Mabingwa wa Soka Barani Afrika Wydad A.C Juan Carlos Garrido Fernández ameichimba mkwara Simba SC kuelekea mchezo wa Mkondo wa Pili wa Robo Fainali, Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.

Simba SC ipo mbele kwa bao 1-0, baada ya mchezo wa Mkondo wa Kwanza uliopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, juzi Jumamosi (April 22), bao likifungwa na Mshambuliaji kutoka DR Congo Jean Othos Baleke.

Kocha Fernandez amesema wamekubali kupoteza mchezo wa Mkondo wa Kwanza dhidi ya Simba SC, na sasa wanachokifanya ni kuhakikisha wanashinda mchezo wa Mkondo wa Pili ambao utapigwa mjini Casablanca-Morocco mwishoni mwa juma hili.

Amesema licha ya matokeo waliyoyapata dhidi ya Simba, bado wana mchezo mwingine wa kujitetea wakiwa nyumbani, na matarajio yake makubwa ni kuhakikisha wanashinda na kutinga Nusu Fainali.

“Tutafanya uchambuzi wa mchezo wetu na Simba SC tuliocheza Dar es salaam- Tanzania ili kuhakikisha kwenye mchezo ujao tunapata matokeo mazuri, tulicheza kipindi cha kwanza tukiwa ugenini, tutacheza kipindi cha pili tukiwa nyumbani Morocco, tuna imani tutafuzu hatua inayofuata.”

“Hali ya hewa ya kucheza saa 10 jioni sio rafiki sana kwetu japokuwa imechangia kwa kiasi chake lakini isiwe sababu, tunajiandaa kwa ajili ya mchezo ujao.” amesema Fernandez baada ya kuwasili Casablanca-Morocco

Wydad A.C itaikaribisha Simba SC katika Uwanja wa Mohammed V mjini Casablanca,  Jumamosi (Aprili 28) ikitakiwa kupata ushindi wa mabao mawili kwa sifuri au zaidi, ili isonge mbele katika hatua ya Nusu Fainali, Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.

Thomas Partey aivimbia Manchester City
Habari Kuu kwenye magazeti ya leo Aprili 24, 2023