Kocha Mkuu wa Wydad Casablanca, Adel Ramzi amewaomba radhi Mashabiki wa klabu hiyo kufuatia kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Mabingwa wa Soka nchini Botswana Jwaneng Galaxy katika mchezo wa michuano ya Ligi ya Mabingwa wa Afrika mwishoni mwa juma lililopita.
Kikosi cha Galaxy kilileta mshtuko katika bara zima la Afrika baada ya kuondoka na pointi zote tatu dhidi ya vigogo hao wa Morocco na Afrika na kuweka historia katika mchezo huo wa Kundi B.
Galaxy, ambao wanaingia kwa mara ya pili katika Hatua ya Makundi ya Ligi ya Mabingwa wa Afrika, imeshtua kwa ushindi huo dhidi ya timu kubwa barani Afrika.
Mshambuliaji wa Galaxy, Thabang Sesinyi alifunga bao hilo pekee katika mchezo huo katika dakika ya 33 na kuifanya timu hiyo kuanza vizuri mbio za kucheza Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa wa Afrika.
Kocha wa Wydad anahisi kuwa kichapo hicho walistahili baada ya wachezaji wake kushindwa kuonesha kiwango chao katika mchezo huo uliochezwa mbele ya mashabiki wa nyumbani.
“Nakubali nimechanganyikiwa na nimefadhaika sana, samahani kwa yote, na wachezaji wangu hawakucheza kwa kujituma zaidi na ndio maana tumepata kipigo hicho, “amesema Kocha Ramzi.
Amesema kuwa pamoja na kipigo hicho, bado ana matumaini ya timu yake kufanya vizuri katika mechi zijazo na kutinga hatua inayofuata.
“Tulifanya makosa na tumeadhibiwa sababu hatukucheza kwa moyo,” amesema kocha huyo.
Kipigo hicho kinaiacha Wydad mkiani mwa msimamo wa Kundi B na timu hiyo inahitaji kurudi kwa haraka wakati watakapokutana na ASEC Mimosa mwishoni mwa juma hili.
ASEC Mimosas ilitoka sare ya bao 1-1 na Simba SC kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam juzi jumamosi (Novemba 25).