Joto la pambano la Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania Bara kati ya Simba Queens dhidi ya Yanga Princess litakalopigwa Ijumaa Uwanja wa Mo Simba Arena, linaendelea kupanda.
Pambano hilo linatarajiwa kuwa na upinzani mkubwa kutokana na matokeo ya mchezo wa mzunguuko wa kwanza, ambao ulimalizika kwa Young Princess kukubali kichapo cha mabao matano kwa sifuri.
Kutokana na hali hiyo Young Princess wanatazamiwa kuingia dimbani wakiwa na lengo la kurekebisha makosa na kulipa kisasi dhidi ya wapinzani wao, ambao kwa sasa wanaongoza msimamo wa Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania Bara kwa kufikisha alama 35, huku Yanga Princess wakiwa nafasi ya tano kwa kumiliki alama 23.
Kocha wa Yanga Princess Edna Lema amesema wanahitaji kufuta ‘uteja’ katika mchezo huo wa keshokutwa kutokana na kufungwa na wapinzani wao kila wanapokutana kwenye Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania.
Edna amesema hawako tayari kupoteza mchezo huo na kuhakikisha wanapambana kupata matokeo mbele ya wapinzani wao, ambao watakua kwenye uwanja wa nyumbani.
“Huu mchezo ni ‘dabi’, ni ngumu itakuwa ya ushindani mkubwa hatuko tayari kupoteza huu mchezo ni muhimu sana kwetu, tunahitaji kufuta uteja wa kufungwa kila tunapocheza nao,” alisema Lema.
“Nawaheshimu wapinzani wetu, tunaendelea na mazoezi kwa kufanyia kazi upungufu wetu wa michezo iliyopita na hadi sasa hatuna mchezaji majeruhi wote wapo fiti,” alisema Lema.
JKT Queens ndio mabingwa watetezi wa ligi hiyo inayoshirikisha timu 12 kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara.