Kocha Mkuu wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans, Miguel Gamond amesema Mashabiki na Wanachama wa klabu hiyo watarajie mabadiliko chanya ya kiuchezaji ambayo yataanza kuonekana kwenye michezo ya Ngao ya Jamii.
Young Africans itacheza na Azam FC Agosti 9, mwaka huu kwenye Uwanja wa CCM Mkwakwani jijini Tanga, ikiwa ni mchezo wa kwanza na mshindi atacheza na timu itakayoshinda katika mchezo mwingine utakaozikutanisha Simba SC dhidi ya Singida Fountain Gate FC kuwania Ngao ya Jamii kwa msimu wa 2023/2024.
Gamondi ambaye anaendelea kuiandaa timu hiyo kwenye kambi yao waliyoiweka Avic Town, Kigamboni Dar es Salaam, amesema baada ya mchezo wao wa kwanza wa kirafiki kwenye Kilele cha Siku ya Mwananchi dhidi ya Kaizer Chiefs, ameendelea kuiongezea makali timu hiyo na kwa sasa wamezidi kuimarika kuelekea kwenye msimu mpya wa mashindano watakayoshiriki.
Amesema mchezo wa kuwania Ngao ya Jamii watakaoanza kucheza Agosti 9, utatoa picha kamili ya kikosi chake na mashabiki wataona mfumo wake wa uchezaji.
“Tunaendelea na program zetu za mazoezi, nafurahishwa na namna wachezaji wangu wanavyojituma na walivyo wepesi kushika maekekezo yangu, tuna mchezo wa Ngao ya Jamii kabla ya kuanza kwa Ligi Kuu, naamini mchezo huo utatoa picha kamili ya kikosi changu namna kilivyobadilika kucheza,” amesema Gamondi.
Amesema anatarajia kucheza mchezo mwingine wa kirafiki kabla ya kwenda Tanga kwenye mchezo huo wa Ngao ya Jamii.
“Nadhani mchezo mwingine wa kirafiki utatuweka sawa tayari kwa mechi ya kuwania Ngao ya Jamii, kwa muda mfupi niliokuwa na timu nimeona ina mashabiki wengi wenye kiu ya mafanikio, naomba waendelee kuisapoti timu yao kwenye michezo ya mashindano yote ambayo tutashiriki,” amesema Gamondi.
Kocha huyo raia wa Argentina, amesema lengo kuu la benchi lake la ufundi msimu huu ni kuhakikisha timu inafanya vizuri zaidi ya msimu uliopita ambao Young Africans ilifanikiwa kucheza fainali ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika, lakini pia ilitetea ubingwa wake wa Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’.