Kocha Msaidizi wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans, Cedric Kaze, aamesema wanajua mchezo wa kesho Jumapili (April 16) dhidi ya Simba SC utakuwa mgumu, lakini watacheza kama fainali kwa ajili ya kuusaka ushindi na kujiimarisha kwenye mbio za kutetea ubingwa wao.

Young Africans itakuwa mgeni wa Simba SC katika Uwanja wa Benjamin Mkapa kuanzia saa 11:00 jioni.

Kaze amesema wameusubiri sana mchezo hio wa dabi na wao kama vinara wa ligi wanahitaji alama tatu na si matokeo mengine licha ya kutambua mchezo huo utakuwa na ushindani unaotokana na ubora wa wapinzani wao.

Kocha huyo kutoka nchini Burundi amesema wanajiandaa kufanya mabadiliko katika sehemu kubwa ya kikosi chao hasa kwenye safu ya ulinzi na hii inatokana na kuimarika kwa Simba katika siku za hivi karibuni.

“Tunafanya mazoezi kulingana na aina ya mchezo tunaenda kucheza, tumekuwa na timu ambayo imekuwa inabadilika kila wakati, mabadiliko yatakuwapo katika maeneo mengi ikiwamo safu ya ulinzi ingawa siyo sasa naweza kutaja nani atakuwapo,” amesema Kaze.

Ameongeza wataongeza umakini katika mchezo huo utakaotoa mwanga wa mbio za ubingwa wa msimu huu lakini pia kujiweka imara kuelekea mchezo wao ya Robo Fainali ya Kombe la Shirikisho Tanzania Bara.

Amesema pia hawataingia kwa kubweteka na rekodi, kwa sababu siku zote ‘dabi’ huwa haitabiriki.

“Ni mchezo ambao unasubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wengi, tunajua nini cha kufanya, dabi siku zote haitabiriki, anayekuja kwa kupambana na kujituma, kufuata vizuri maelekezo ya walimu ndiyo anashinda, kuongoza kwetu ligi na nafasi tuliyonayo haitupi au kutusaidia lolote kupata ushindi, kitu kikubwa ni kujituma na kucheza kama fainali, hilo tunalijua na tupo tayari,” amesema Kaze

Hadi sasa Young Africans inaongoza msimamo wa Ligi Kuu kwa kuwa na alama 68, huku Simba SC ikishika nafasi ya pili kwa kumiliki alama 60 na timu zote zimeshacheza michezo 25.

https://www.youtube.com/watch?v=OO1CkmCuS-I&t=3s

Juma Mgunda: Tupo tayari kupambana
Wanne wafariki ugonjwa usiojulikana, Wizara yatoa tahadhari