Kocha Mkuu wa Young Africans Nasreddine Nabi, amesema anafurahi kuona kikosi chake kimeendelea kuimarika kwa ajili ya kutimiza malengo ya kuibuka na ushindi katika mchezo wao dhidi ya Mbeya City utakaochezwa keshokutwa Jumamosi (Februari 05), Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.
Nabi aemsema hesabu zake kuelekea mchezo huo zinakwenda vyema na kila mchezaji anaonekana yuko tayari kuisaidia timu ipate ushindi.
Hata hivyo, kocha huyo kutoka nchini Tunisia amesema wachezaji wake wanatakiwa kuongeza umakini kufuatia baadhi ya matukio anayoyaona wanapokuwa katika mazoezi kwa sababu anafahamu wapinzani wao pia wamejipanga.
Amesema malengo yao makubwa ni kuhakikisha msimu huu wanabeba ubingwa kwa sababu hiyo kwao kila mechi wanayocheza ni sawa na fainali.
“Kikubwa ambacho tunahitaji ni alama tatu muhimu, ili kupata alama ni lazima tushinde mchezo wetu. Ushindani ni mkubwa na kila timu inafanya kazi kubwa kusaka pointi, kazi ni kubwa na wachezaji watahakikisha wanatekeleza kile tunachokifundisha kwenye mazoezi kwa kukipeleka uwanjani,” amesema Nabi.
Amesema wapinzani wao wamekuwa na kikosi imara zaidi msimu huu na wamejiandaa kukutana na ushindani mkubwa katika mechi hiyo kutokana na mabadiliko yaliyofanywa kwenye kikosi chao.
“Tunazihitaji alama , nimeandaa kikosi changu kwa ajili ya kupata matokeo mazuri, hakuna mechi ndogo, hakuna timu ndogo, ligi hii ni ngumu, kikubwa ni kuongeza utulivu ili kujiimarisha katika mbio za ubingwa, tunapokuwa na mpira na kujipanga pale unapokuwa kwa wapinzani wetu, ” Ameongeza Nabi.
Young Africans inaongoza msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na alama 35, huku wapinzani wao Mbeya City wakishika nafasi ya tatu kwa kufikisha alama 22, baadaya kucheza michezo 13 mpaka sasa.