Kocha Mkuu wa Young Africans Nasreddine Nabi, ameshindwa kujizuia kwa wachezaji wake na kuwakoromea kutokana na kumruhusu Henock Inonga kupiga kichwa akiwa hajakabwa na kufunga bao la kwanza, juzi Jumapili (April 16).
Young Africans iliyokuwa mgeni wa mchezo huo uliopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, ilikubali kupoteza mchezo huo dhidi ya Simba SC kwa mabao 2-0, kupitia kwa wafungaji Inonga na Kibu Denis.
Taarifa kutoka kwenye kambi ya Young Africans zinaeleza kuwa Kocha Nabi hakufurahishwa na kitendo cha wachezaji wake kumruhusu Inonga kupiga kichwa cha wazi jambo lililowafanya kupoteza kujiamini mapema.
“Kiliwaka sana kwa mabeki na viungo wa Young Africans, baada ya Nabi kuhoji kwa nini walimuachia Inonga kupiga kichwa akitokea mbali bila kukabwa, jambo ambalo yeye aliliita kama udhaifu mkubwa,” zimeeleza taarifa hizo
Akizungumza baada ya mchezo huo, Kocha Nabi alikubali wazi kuvurugwa na bao la kwanza la Simba SC lililofungwa na Inonga, ambapo alisema hakufurahishwa kabisa na uzembe huo.