Kocha mkuu wa Young Africans Zlatko Karmpotic, amesema anatarajia makubwa kutoka kwa kiungo Carlos Fernandes Carlinhos, ambaye Jumapili, Septemba 13 aliisaidia klabu hiyo kuchomoza na ushindi wa bao moja kwa sifuri dhidi ya Mbeya City.
Carlinhos alipiga kona iliyounganishwa kwa kichwa na beki kutoka Ghana Lamine Moro dakika ya 87 na kwenda moja kwa moja nyavuni na kuifanya Young Africans kukusanya alama tatu za mchezo huo, uliochezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Kocha Karmpotic amesema licha ya mchezaji huyo kuonesha ubora wa kutumia vema mipira iliyokufa kwenye mchezo dhidi ya Mbeya City, bado hawajawa tayari kuingia kwenye mfumo, hivyo anaendelea kumuandaa ili arejee kwenye makali yake.
“Carlinhos ni mchezaji mzuri bado namuaandaa sitaki kumuua, ila amekuwa akilazimika kutokea benchi, namuaandaa ili afiti kwenye kikosi kwani ana muda mrefu hajacheza mpira kwao Angola ambako alikaa kwa zaidi ya miezi mitano kwa sababu ya Corona,” amesema Karmpotic.
Pia kocha huyo kutoka nchini Serbia aliwagusia wachezaji wengine akiwemo Yacouba Sogne, akisema naye hajawa kwenye kiwango chake, kwani amekaa bila kucheza mpira kwa miezi minne, hivyo sio kazi rahisi kwa kocha kukitengeneza kikosi kwa mara moja anatakiwa kupewa muda wa kutosha kutengeneza muunganiko.
Young Africans mwishoni mwa juma hili wataendelea na harakati za kulisaka taji la Tanzania Bara msimu wa 2020/21, kwa kupambana dhidi ya Kagera Sugar kwenye Dimba la Kaitaba mjini Bukoba mkoani Kagera.