Ni Rasmi Kocha Mkuu wa Simba SC Zoran Maki amewaondoa kikosini mwake Washambuliaji wawili wa Kimataifa Chriss Mugalu (DR Congo) na Meddie Kagere (Rwanda), huku Kiungo Thadeo Lwanga (Uganda) akijumuishwa kwenye mpango huo.
Kocha Zoran alipewa jukumu hilo na Uongozi wa Simba SC, ili kubaki na idadi kamili ya wachezahi 12 wa Kigeni, ambao wanatakiwa kusajiliwa Kikanuni katika Ligi ya Tanzania Bara.
Taarifa kutoka Misri, zinasema Zoran ametumia siku 13 kuanzia Julai 15, walipoanza kambi akiwasoma wachezaji wake kisha kugundua nani anaweza kuisaidia Simba msimu ujao.
Baada ya Kikosi cha Simba SC kupoteza mchezo wa Kimataifa wa Kirafiki dhidi ya Haras El Hodoud juzi Jumatano (Julai 27), Zoran aliwapa taarifa mabosi wa klabu hiyo akiwaambia hatakubaliana na ubora wa washambuliaji Chris Mugalu na Meddie Kagere.
Mbali na Mugalu na Kagere ambao ndio walikuwa washambuliaji wawili pekee wa Kigeni walioitumikia Simba SC msimu uliopita, pia akakata jina la kiungo Thadeo Lwanga.
Tayari mastaa hao wameshaondoka kambini kurejea Dar es salaam kwa ajili ya kumalizana na mabosi wa Simba SC, huku Kocha Zoran akihitaji kubaki na wachezaji wengine pekee.
Kilichowashtua zaidi mabosi wa Simba ni kwamba Zoran hajamaliza panga hilo kwani kuna mastaa wengine watatu nao wanaweza kufuata huku mmoja kati ya hao akiwemo nyota mpya kabisa aliyesajiliwa msimu huu.
“Kuna mchezaji mpya katuambia naye hakubaliani na ubora wake lakini tayari tumeshamsajili kwa fedha nyingi hili limetushtua sana tunasubiri,” amesema mmoja wa mabosi wa juu wa Simba SC.
Habari njema kwa Simba ni kwamba kiungo Sadio Kanoute ambaye alikwama kujiunga na kambi kutokana na pasi yake kujaa yuko katika hatua za mwisho kujiunga na wenzake akisubiri visa pekee. Kanoute tayari ameshatua Tanzania akisubiri taratibu za safari.