Kocha Mkuu wa Simba SC Zoran Maki atakua na kazi ya kukata majina matatu ya wachezaji wa Kigeni endapo klabu hiyo itakamilisha usajili wa wachezaji wengine watatu katika Dirisha hili la Usajili.
Simba SC imetangaza kufanya usajili wa wachezaji wengine watatu wa Kimataifa, baada ya kukamilisha na kuwatambulisha Wachezaji watatu katika kipindi hiki ambao ni Moses Phiri (Zambia) Victor Akpan (Nigeria) na Augustine Okrah (Ghana).
Wachezaji wanaotajwa huenda wakatangazwa na Simba SC baada ya mipango ya usajili wao kukamilishwa kabla ya Dirisha kufungwa ni Beki Mohamed Outtara (Ivory Coast), Kiungo Mshambuliaji Nelson Okwa (Nigeria) na Mshambuliaji Cezer Lobi Monzaki (Jamhuri ya Afrika ya Kati).
Simba SC ilikuwa na jumla ya wachezaji 12 wa kimataifa na tayari wameshaondoka wachezaji watatu (Bwalya, Wawa, Morrison) na waliobaki hadi sasa ni 12 ambao wataungana na wengine watatu watakaotangazwa baadae.
Ila wachezaji wa zamani ambao Uongozi ulipanga kuwaacha ni Meddie Kagere, Thadeo Lwanga huku mvutano ukiwa mkubwa kwa Chris Mugalu viongozi wakitofautiana wengine wakisema apewe msimu mmoja ili Peter Banda atolewe kwa mkopo au Sadio Kanoute auzwe.
Ila kwa sasa jukumu hilo ameachiwa kocha mkuu Zoran Maki kuamua yeye nani abaki nani aondoke kwa wachezaji hao watano (Kagere, Lwanga, Mugalu, Banda, Kanoute) na iwapo dili la Manzoki likisumbua wanaweza kuachana na wachezaji wawili na Manzoki atajiunga na Simba Dirisha Dogo.
Wachezaji wa Kimataifa waliopo Kambini kwa sasa ni Joash Onyango (Kenya), Hennock Inonga (DRC), Victor Akpar (Nigeria), Taddeo Lwanga (Uganda), Sadio Kanoute (Mali), Clatous Chama (Zambia), Augustine Okrah (Ghana), Pape Sakho (Senegal), Peter Banda (Malawi), Moses Phiri (Zambia), Chris Mugalu (DRC) na Meddie Kagere (Rwanda).