Siku moja baada ya Shirikisho La Soka Barani Ulaya (UEFA) kupanga ratiba ya michezo ya hatua ya mtoano ya Ligi ya Mabingwa barani humo, meneja wa FC Barcelona Ronald Koeman, ametuma ujumbe kwa mabingwa wa soka nchini Ufaransa Paris Saint-Germain (PSG).

FC Barcelona wamepangwa kukutana na PSG kwenye hatua hiyo, huku mchezo wa kwanza ukitarajiwa kuchezwa Camp Nou (Hispania) Februari 16, na mchezo wa pili utachezwa jijini Paris Ufaransa, Machi 10.

Koeman amesema wameipokea kwa mikono miwili ratiba ya hatua hiyo, na anaamini mpambano utakua na vuta ni kuvute, kutokana na wapinzani wao kuwa na wachezaji wenye viwango vya hali ya juu.

Amesema wanaiheshimu PSG kama mshindani wao, na katu hawatabweteka kwa kuamini historia ya michuano ya Ulaya imekua ikiwabeba mara kwa mara, licha ya msimu uliopita kukabiliwa na changamoto ya kuondoshwa aibu ya kufungwa mabao manane kwa mbili dhidi ya FC Bayern Munich.

“PSG ni timu yenye nguvu, lakini pia ni ngumu kwao kwa sababu sisi pia ni timu ngumu na naona ni sawa kabisa.”

“Katika miaka ya hivi karibuni wametumia pesa nyingi kuijenga timu ambayo inaweza kupigania mataji makubwa kama Ligi ya Mabingwa. Msimu uliopita walifika fainali, na ni timu ambayo itaendelea kuwepo.” Amesema Ronald Koeman.

Msimu uliopita PSG walifikia hatua ya fainali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya lakini walikwama mbele ya mabingwa FC Bayern Munich, lakini wamebarikiwa kuwa na vipaji vya washambuliaji wenye uwezo mkubwa wakiwemo Neymar Junior na Kylian Mbappe.

Somalia yavunja uhusiano wa kidiplomasia na Kenya
Tanzia: Mzee Jengua afariki dunia