Mwanamuziki nguli wa muziki wa Rhumba na Soukous kutoka nchini Congo Antoine Christophe Mumba maarufu Koffi Olomide amehukumiwa na Mahakama ya rufaa nchini Ufaransa kwa kosa la kuwashikilia wanawake bila hiari yao na imemuondolea kosa la unyanyasaji wa kingono.
Mahakama ilibatilisha uamuzi wa mwaka 2019 uliomkuta na hatia ya ubakaji wa mmoja wa wachezaji densi alipokuwa na umri wa miaka 15.
Hukumu yake inakuja baada ya hatia ya kuwanyima wanawake uhuru wao katika jumba la kifahari huko Paris huku moja kati wahanga akibainisha kufanyiwa vitendo hivyo wakiwa hotelini, kwenye gari na hata kwenye chumba cha studio ya kurekodia muziki, kati ya miaka ya 2002 na 2006
Kofii atatumikia kifungo cha miezi 18 na kuwalipa fidia wanawake wote aliotuhumiwa kuwasumbua kingono pia atalipa faini ya dola $11,000-36,000 kwa kila mcheza densi aliekua nae wakati huo.
Wakati wa hukumu hiyo inatangazwa katika mahakama ya Versailles Ufaransa, inaelezwa kuwa msanii huyo hakuwepo mahakamani hapo.
Licha ya hukumu ya miaka takribani minane iliyoombwa na upande wa mashtaka kwenda kwa Koffi, kwa mujibu wa kanuni za hukumu hiyo ni kuwa mwanamuziki huyo amewekwa katika kipindi cha uangalizi mkali kwa muda wa miaka mitatu mfululizo Ikiwa ni pamoja na kuwekewa kizuizi cha kuwasiliana na wahanga wa matukio aliyoyafanya dhidi yao.
Kwa mujibu wa waendesha mashtaka wa kesi hiyo, wanaeleza kuwa kiasi cha pesa kinachotokana na faini hiyo ya Euro 72,000. Kitagawiwa kwa waathirika wanne wa matukio ya unyanyasaji wa kingono yaliyofanywa na Koffi Olomide ambao kati yao wapo waliowahi kuwa wanenguaji katika nyimbo zake.
Hii si mara ya kwanza kwa nyota huyo mwenye umri wa miaka 65 kukutwa na hatia za kuhusishwa na matukio mbali mbali yenye taswira ya unyayasaji.
• Ikumbukwe mwaka 2018, serikali ya Zambia ilitoa amri ya Koffi kuwekwa chini ya ulinzi baada ya kumshambulia mpiga picha.
• Mwaka 2012 alipatikana na hatia ya kumshambulia mtayarishaji wake na akapatiwa adhabu ya kifungo cha miezi mitatu Jela.
• Na mwaka 2008 pia aliwahi kushtakiwa kwa kumpiga teke mpiga picha kutoka kituo cha televisheni cha RTGA cha nchini Kongo na kumvunjia Kamera yake, ilikuwa kwenye tamasha, japo baadaye walipatanishwa na kufikia muafaka.