Uongozi wa Klabu ya Burnley itakayoshiriki Ligi Kuu ya England msimau ujao wa 2023/24 imemzawadia Meneja wa kikosi chao Vincent Kompany mkataba mpya wa miaka mitano, baada ya kuipandisha timu hiyo kutoka Ligi ya Championship.
Beki huyo wa zamani wa Manchester City aliipandisha timu hiyo hadi EPL katika msimu wake wa kwanza, baada ya kuwa Meneja wa kikosi kwenye dimba la pale Turf Moor.
Amekuwa akihusishwa na nafasi nyingi za ligi kuu zikiwamo Chelsea na Tottenham Hotspur, lakini sasa ameweka mustakabali wake kwa Clarets hao hadi mwaka 2028.
Baada ya kusaini mkataba wa muda mrefu, Mbelgiji huyo amesema: “Burnley walijisikia vizuri tangu mwanzo kwa hiyo ninahisi sawa kusaini miaka mitano ijayo.
“Pamoja na mashabiki tumeufanya Uwanja wa Turf Moor kuwa ngome tena na tunaendelea kutazamia siku zijazo na kazi ya kuifanya Burnley kuwa bora kwa kila hatua.” Kompany alichukua nafasi ya Sean Dyche maji ya joto yaliyopita baada ya klabu hiyo kushuka daraja.