Serikali nchini, imetoa Shilingi 900,000,000 Milioni kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa Hospitali ya Mji wa Kondoa, ili kuboresha utoaji wa huduma za afya kwa kujenga majengo matatu ambayo ni Jengo la wazazi, Jengo la upasuaji na Jengo la kuhifadhia maiti ambayo ujenzi wake unaendelea..
Haya yamebainishwa na Mkurugenzi wa Mji Kondoa, Paul Sweya wakati akisoma taarifa ya hatua za ujenzi na ukarabati wa majengo matatu mbele ya Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma Bw. Ally Gugu ambae yuko kwenye ziara ya kukagua utekezaji wa miradi ya maendeleo katika Wilaya ya Kondoa.
Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma, Ally Gugu akiongea mara baada ya taarifa hiyo amesema ni vyema ujenzi wa miradi hiyo kukamilika kwa wakati na kuelekeza kuwa kufikia Juni 15, 2023 ujenzi uwe umekamilika nakuwataka pia kukarabati wodi ya Watoto na kujenga njia viunganishi.
Halmashauri ya Mji wa Kondoa inaendelea na utekelezaji wa miradi mingine ikiwa ni pamoja na Ujenzi wa Kituo cha Afya Serya unaogharimu Shilingi 500,000,000 milioni zitakazojenga Maabara, Jengo la Mapokezi ya Wagonjwa wa nje, Jengo la Upasuaji na Jengo la Wazazi pamoja na Zahanati ya Ausia na Chandimo.