Kongamano la Kimataifa la Jinsia na Usawa Katika Jamii lililoandaliwa na Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (DUCE) linatarajiwa kufanyika Aprili 27 mpaka 28 mwaka huu chuoni hapo.
Hayo yamesemwa mapema hii leo Jijini Dar es Salaam na Afisa Habari, Elimu na Mawasiliano wa Chuo hicho, Lila Mandu alipokuwa akiongea na waandishi wa habari kuhusu lengo la kongamano hilo.
Amesema kuwa lengo kuu la kongamano hilo ni kuchunguza kwa kina masuala mbalimbali ya kijinsia pamoja na kubaini mbinu bora za kuondoa ukosefu wa usawa wa jinsia katika muktadha wa Taasisi za Elimu ya Juu.
“Tutatathmini sababu na changamoto zinazosababisha ukosefu wa usawa wa kijinsia katika Taasisi za Elimu ya Juu kwa kutumia mifano mizuri kutoka Taasisi zingine ambazo zinajitahidi kuhamasisha usawa na haki za wanawake na wanaume pia,” amesema Mandu.
Aidha, ameongeza kuwa kongamano hilo litabainisha fursa za kimkakati katika kuwahusisha wadau wa masuala ya jinsia katika kuhamasisha usawa na haki za watu wote ambapo litakuwa na washiriki 140.
Kwa upande wake, Mratibu Kitengo cha Jinsia DUCE, Fatma Hamad amesema kuwa licha ya maovu wanayotendewa wanawake kuendelea kujitokeza hapa nchini, pia litasaidia kutoa elimu ya jinsia na usawa ili kusaidia Serikali na wananchi kwa ujumla kuondokana na tatizo hilo.
Hata hivyo, Chuo hicho pamoja na waandaaji wa kongamano hilo wamealika wadau mbalimbali wa masuala ya jinsia, wasomi, waandishi wa habari na wananchi kwa ujumla kushiriki katika kongamano hilo.