Kiongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe na wenzake zaidi ya 10, wanadaiwa kukamatwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza usiku wa kuamkia leo Jumatano, Julai 21, 2021, katika Hotel ya Kingdom jijini humo.

Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema amewataja baadhi ya waliokamataa ni, Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho, John Heche, Mwenyekiti wa Baraza la Vijana (Bavicha), John Pambalu na Mhadhiri mwandamizi wa zamani wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Azaveri Lwaitama.

“Polisi walifika hotelini hapo na kuwakamata Mbowe na wengine 11 majira ya saa nane usiku. Wamepelekwa Central Polisi ila Mbowe pekee ndio hatujui amepelekwa wapi. Tunaendelea kufuatilia kujua yupo wapi,” amesema Mrema.

Kongamano hilo lililozuiwa na polisi Jumamosi iliyopita, lilielezwa na Mbowe kwamba litafanyika leo Jumatano huku Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Robert Gabriel akipiga marufuku mikusanyiko isiyokuwa na kibali maalum.

Itakumbukwa Julai 20, 2021 Rc Gabriel alitoa zuio la mikusanyiko akidai ni jitihada za kujikinga na maambukizi ya virusi vya corona ambavyo mkoani humo vimeshamili. 

Hata hivyo, Chadema kupitia kwa Mrema walisema, kongomano hilo litafanyika kwani limezingatia tahadhari ya corona ikiwemo kila mshiriki kuvaa barakoa na kunawa na maji tiririka.

Naibu Waziri amuonya mkandarasi ''Hatutaongeza muda''
Mwingine aondoka AS Vita Club