Boniface Gideon – Tanga.
Zaidi ya wanafunzi 60 wa shule Sekondari kutoka katika Mikoa mbalimbali ya Tanzania wameshiriki kikamilifu Kongamano la saba la Sayansi na Teknolojia huku wakiaswa kujiepusha na mambo ya uzinzi, ukahaba na usagaji na badala yake wajitunze huku wakisoma kwa bidii, ili wafikie malengo yao na wazazi wafurahi na kuwapatia baraka maishani.
Rai hiyo imetolewa na Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya jiji la Tanga, Dkt. Sipora Liana wakati wa ufunguzi wa Kongamano hilo na kulipongeza shirika la Botna ambalo ni wafadhili wa miradi mbalimbali inayotekelezwa jijini humo, ikiwemo kituo cha Stem Park pamoja, Walimu wanaowafundisha Vijana na Wanafunzi, huku akiwataka pia kuwafundisha maadili mema.
“Jilindeni vijana na jitunzeni msome kwa bidii ili mfikie lengo wazazi wenu wafurahi na mtapata baraka nyingi kwa wazazi , Mambo ya uzinzi , ukahaba ushoga , usagaji achaneni nayo zingatieni masomo yenu mfikie malengo yenu nawatakia kila la kheri” alisema Dkt. Liana.
Aidha, Dkt. Liana ameongeza kuwa, “tunatambua mchango mkubwa wa botna foundation ni mengi wametusaidia katika nyaja ya kielimu kijamii na hata afya pia wametoa Madawati ya shule za msingi Milioni 286.3 , Mambo ya usalama barabarani wametoa milioni 442.5 , wamejengea uwezo kiuchumi vijana milioni 434.9 hii miradi yote ni maendeleo makubwa ndani ya jiji la Tanga kwa ajili ya wananchi.”
Kwa upande wake Mratibu wa Kongamano hilo, Dkt. Isaya Ipyana alisema wamekuwa wakiwaelekeza wanafunzi hao namna ya kukabiliana na changamoto ya mabadiliko ya tabia nchi kwa kutumia elimu ya sayansi, Teknolojia, uhandisi na mahesabu ambayo wamekuwa wakifundishwa kwa nadharia.
“Wapo ambao waliweza kutengeneza ndege nyuki (drones), wapo ambao waliweza kutengeneza mitambo kwa ajili ya gesi, kwahiyo nia kubwa ni kuhakikisha yale waliyoweza kujifunza darasani kwa nadharia wajifunze kwa vitendo na tunashukuru kwamba wamefanikiwa,” alisema Dkt. Ipyana.
Akizungumza kwa niaba ya Botna Foundation, Mbogolo Philoteus alisema shirika hilo linaamini kumuandaa kijana katika karne ya sasa na ijayo, kwa ajili ya kuingia kwenye soko la kiushindani hatua ambayo itawasaidia kutojiingiza katika vitendo vya mmomonyoko wa maadili na kuwafanya kutotimiza ndoto zao kielimu.
Kongamano hilo liliandaliwa na Kituo Cha Sayansi Tanga Stem Park na limeonesha umahiri katika kukabiliana na changamoto ya mabadiliko ya tabia ya Nchi kupitia sayansi, Uhandisi na Hisabati.