Kuelekea mchezo wao wa leo Ijumaa (Desemba 08) dhidi ya Medeama SC, uongozi wa Young Africans umechimba mkwara mzito kuwa umefanya maandalizi ya kutosha kuibuka na ushindi, huku wakiweka wazi kuwa uwepo wa Mshambuliaji wao kutoka Ghana, Hafiz Konkon ambaye alicheza nchini humo msimu uliopita umewaongezea taarifa muhimu.
Young Africans ambao wamepangwa Kundi D la michuano hiyo mpaka sasa katika michezo yao miwili ya kwanza wamefanikiwa kukusanya pointi moja tu, hali ambayo inawafanya wabuluze mkia, huku mchezo huo ukitarajiwa kuwa mchezo wa tatu kwao.
Young Africans wataingia katika mchezo huo wakiwa na kumbukumbu ya matokeo ya sare katika mchezo wao uliopita dhidi ya Al Ahly, ambao uliopigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es salaam.
Ofisa Habari wa Young Africans, Ali Kamwe amesema: “Maandalizi ya kikosi chetu yanaenda vizuri kuelekea mchezo huu muhimu dhidi ya Medeama, tumetoka kupata matokeo ya sare dhidi ya Al Ahly na mpaka sasa tumepata pointi moja tu, katika michezo miwili ya kwanza.
“Uzuri kwetu kuelekea mchezo huu tuna hazina ya mchezaji ambaye anayajua vizuri mazingira ya hapa ambaye ni Mshambuliaji wetu, Konkoni ambaye amekuwa sehemu ya programu za maandalizi kutokana na uzoefu wake. Tunajua utakuwa mchezo mgumu lakini malengo yetu ni kupata pointi tatu muhimu.”