China imesema kuwa imeshangazwa na taarifa kutoka kwa bunge la Kenya kuwa Kontena lililokuwa na vifaa vilivyotolewa kama msaada kutoka China na kuwasili siku ya Jumanne na kufunguliwa na maafisa wa bunge la Kenya lilikuwa tupu.
Taarifa nchini humo zinasema kuwa kontena hilo lenye vifaa vya msaada lilipelekwa makao makuu ya bunge liliwasili likiwa halina kitu ndani.
Akizungumza na shirika la Utangazaji la Uingereza BBC, msemaji wa jeshi la polisi nchini Kenya, Charles Owino kuhusu taarifa za kontena hilo kuwasili kutoka nchini China na kupelekwa katika viwanja vya bunge likiwa tupu, amesema hana taarifa kabisa kuhusu taarifa hizo isipokuwa kupitia mitandao.
”Kwa kawaida huwa tunapata taarifa kutoka kwa mkuu wa polisi na sijui kama ni mambo ya mitandao ya kijamii ama ni kweli kwa sababu sijapata taarifa kwa mkuu wa upelelezi hivyo pengine niulizie halafu baadaye tuweze kuzungumza,”amesema Owino
Katika hatua nyingine, uchunguzi unaripotiwa kuidhinishwa kupitia idara ya makosa ya jinai nchini humo katika kile kinachotajwa na vyombo vya habari vya Kenya kuwa ni kubaini mazingira yaliyojitokeza ya kontena hilo kutoka China kuwasili Kenya likiwa tupu.
Vifaa vilivyoorodheshwa kupotea ndani ya kontena hilo ni pamoja na kompyuta mpakato, na projekta zilikuwa msaada kutoka Bunge la Taifa la China na mzigo huo ulipaswa kufikishwa Kenya kupitia ubalozi wa China nchini Kenya.
Katika taarifa iliyowasilishwa siku ya Jumatano, Karani wa Bunge la Kenya, Michael Sialai amethibitisha kuwa kontena lililowekwa nembo ya ‘mizigo ya kidiplomasia’ liliwasili siku ya Jumanne, tarehe 30 mwezi Julai mwaka 2019 kama ilivyotarajiwa lakini baada ya kufunguliwa, hakukuwa na kitu ndani yake, Televisheni ya Citizen ya Kenya imeripoti.
”Kweli Kontena liliwasili katika viwanja vya bunge tarehe 30 mwezi Julai, 2019, ambapo niliwateua maafisa kadhaa kutoka kwenye bunge waweze kuthibitisha mzigo kwa ulinganifu na kile kilichoelezwa kuwasilishwa na ubalozi wa China, baada ya kufungua kontena, ilithibitishwa kuwa lilikuwa tupu. Wakala na maafisa wetu kwa pamoja walinifikishia suala hilo na kuamua kuwa maafisa wa DCI wapatiwe taarifa hiyo, suala ambalo lilifanyika ipasavyo”ilieleza taarifa ya Sialai