Rais wa Shirikisho la Soka Duniani ‘FIFA’ Gianni Infantino amesema nchi Korea Kaskazini ina nafasi ya kuandaa Kombe la Dunia siku zijazo, kwani anatazamia kuleta ‘mabadiliko ya kweli’.
Infantino ambaye anatazamiwa kuchaguliwa tena kwa muhula wa tatu, alifichua kwamba taifa lolote linastahili kuwa mwenyeji wa hafla hizo, akiongeza kuwa shirika lake linataka kusaidia kuunganisha ulimwengu.
Rais huyo mzaliwa wa Uswizi pia alikiri kuzuru Korea Kaskazini siku za nyuma katika jaribio la kutathmini iwapo taifa hilo litakuwa tayari kuandaa mashindano ya Wanawake pamoja na majirani zao Korea Kusini.
“FIFA ni shirikisho la Soka Duniani, sisi ni watu wa soka, si wanasiasa, na tunataka kuleta watu pamoja.”
“Nchi yoyote inaweza kuandaa Mashindano makubwa ya Soka. Ikiwa Korea Kaskazini inataka kuandaa kitu. Kweli nilienda Korea Kaskazini miaka kadhaa iliyopita kuwauliza Wakorea Kaskazini kama walikuwa tayari kuandaa sehemu ya Kombe la Dunia kwa Wanawake na Korea Kusini.”
“Sawa, sikufanikiwa, ni wazi, lakini ningeenda mara nyingine ni asilimia 100 kama ingesaidia.”
“Ushirikiano pekee ndio unaweza kuleta mabadiliko ya kweli. Sisi ni Shirikisho la Kimataifa na tunataka kubaki kuwa Shirikisho linalounganisha Dunia.”
Ikiorodheshwa ya 112 duniani, Korea Kaskazini haijaonekana kwenye michuano mikubwa zaidi ya soka tangu mwaka 2010 wakati wa Fainali za Kombe la Dunia zilizofanyika Afrika Kusini, ikiwa ni Fainali zao za pili baada ya zile zilizofanyika nchini England mwaka 1966.