Serikali ya Korea Kaskazini imesema kuwa Marekani ilipoteza nafasi ya dhahabu katika mazungumzo kati ya Rais Donald Trump na kiongozi wao, Kim Jong Un mwezi uliopita nchini Vietnam, hivyo wao wataendelea na maisha yao ya kawaida.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Korea Kaskazini, Choe Sun-hui alipokuwa akizungumza na wanadiplomasia wa nchi mbalimbali.
“Hatuna nia yoyote ya kujibana kwenye mahitaji ya Marekani kwa namna yoyote, na hatuna nia ya kuendelea na mazungumzo ya aina hii,” Shirika la Habari la Urusi la TASS linamkariri, naibu waziri Choe.
Choe alieleza kuwa Kim Jong Un mwenyewe atazungumzia kwa undani kuhusu uamuzi wa nchi hiyo baada ya kuvunjika kwa mazungumzo yake na Trump.
Kwa mujibu wa Trump, walishindwa kuendelea na mazungumzo baada ya Korea Kaskazini kutaka iondolewe vikwazo vyote kama sharti la kuharibu vinu vyote vya makombora ya nyuklia.
Hata hivyo, upande wa Korea Kaskazini ulikanusha maelezo hayo ya Trump na kueleza kuwa iliomba kuondolewa vikwazo katika sehemu chache zitakazowasaidia wananchi wake wa kawaida kuendesha maisha yao kwa ubora zaidi hasa kiuchumi.
Inaelezwa kuwa baada ya mkutano huo kuvunjika, Korea Kaskazini imeanza kuandaa mpango mwingine wa kufanya majaribio ya makombora yake, hatua ambayo Trump amedai kama itakuwa kweli itamvunja moyo kwani anaamini bado kuna nafasi nyingine.